Na Winfrida Mtoi, Gazetini
ZIARA za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alizofanya nchini Uganda na Ethiopia zimefungua fursa mpya za ushirikiano katika biashara, uchumi, nishati na afya, zikiwemo hatua za kupanua masoko, kuharakisha miradi ya kimkakati na kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 24, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu amesema ziara ya Uganda ililenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, huku ikizaa matokeo katika maeneo matano muhimu.

Amesema maeneo hayo ni kuondoa vikwazo vya biashara na kupanua masoko, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati, kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika amani na usalama, pamoja na kukuza viwanda na uzalishaji wa pamoja.
Katika sekta ya nishati, amesema ziara hiyo imechochea juhudi za kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao kwa sasa umefikia asilimia 93.9 ya utekelezaji.
Kwa upande wa usafiri na usafirishaji, amesema ushirikiano huo unahusisha mkataba wa mfumo wa ushirikiano wa kuendeleza reli ya kisasa, hatua inayolenga kuboresha muunganiko wa miundombinu na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
Aidha, amesema katika ziara hiyo Rais Samia alishiriki uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha magari nchini Uganda, hatua inayolenga kukuza viwanda na uzalishaji wa pamoja.
Kuhusu ziara ya Ethiopia iliyofanyika Novemba 22 na 23, 2026, Machumu amesema Rais Samia alishiriki ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), ambapo pia alizindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika wa mwaka 2026 hadi 2030.
Amesema mpango huo unahusisha nchi zote 55 wanachama wa Umoja wa Afrika na unatokana na jukumu alilopewa Rais Samia na wakuu wa nchi na Serikali za Umoja huo, Februari 2026, la kuwa kinara wa kuendeleza ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.
“Katika kutekeleza jukumu hilo, tarehe 23, yaani jana, Mheshimiwa Rais alizindua mpango elekezi wa kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika wa mwaka 2026 mpaka 2030, unaohusu nchi zote 55 za Umoja wa Afrika. Mpango huo una malengo matatu yanayojulikana kama sifuri tatu,” amesema Machumu.

Akizungumzia hatua za utekelezaji wa mpango huo, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Tanzania itatoa fursa za mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu wa afya kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuimarisha huduma za afya ya uzazi.
Amesema mafunzo hayo yatajikita katika maeneo muhimu yakiwemo ukunga, magonjwa ya wanawake na uzazi, pamoja na usingizi na ganzi, ambayo ni sehemu muhimu katika utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.


