Na Winifrida Mtoi, Gazetini-DAR
TANZANIA imeingia makubaliano ya udhamini wa matangazo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yatakayoiwezesha kutumia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kutangaza vivutio vyake vya utalii kimataifa.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa leo, Novemba 25, 2026, kati ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na CAF, yanalenga kutumia nguvu ya soka kuongeza mwonekano wa Tanzania duniani, kuvutia watalii na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya utalii ikiendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa nchi, ikichangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2025 Tanzania ilipokea watalii 2,294,495 na kupata mapato ya Dola za Marekani bilioni 4.41, sawa na ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Sekta hiyo pia inatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa takribani Watanzania milioni 3.6, hivyo kuitangaza kupitia AFCON ni fursa ya kukuza utalii na kuongeza manufaa yake kwa wananchi.


