16 C
New York

Koffi Olomide: Chanzo cha vita yake na Fally Ipupa, Ferre Gola – [4]

Published:

KINSHASA, DRC

KATIKA sehemu iliyopita, tuliona Koffi akiwa na bifu zito na mkali mwenzake, Papa Wemba. Hata hivyo, huo haukuwa ugomvi pekee kati yake na wasanii wengine wakubwa nchini DRC.

Kwa nyakati tofauti, Koffi aliwahi kukwaruzana kwa vita ya maneno na hata kutungiana ngoma za kupigana vijembe na JB Mpiana na Werrason.

Hata hivyo, hapa tunaangazia ugomvi wake na vijana wawili, Fally Ipupa, na Ferre Gola, ambao kwa sasa ni kama ndiyo walioushika muziki wa Rhumba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo [DRC].

Kwa Fally Ipupa, alifanya kazi na Bendi ya Koffi, Quartier Latin International, kwa miaka takribani saba kuanzia mwaka 1999 akiwa mwimbaji, mtunzi na dansa.

Mwaka 2006, Fally Ipupa aliamua kung’atuka kwenye Bendi hiyo na kuanza kufanya kazi akiwa msanii wa kujitegemea [solo artist].

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa chanzo ni ugomvi wake na Koffi, ambapo Fally Ipupa alionesha kuchoshwa na ‘udikteta’ wa bosi wake huyo ndani ya bendi.

Koffi alijibu shutuma hizo akisema Fally Ipupa ni miongoni mwa wanamuziki wengi, ambao wameshindwa kulipa fadhila baada ya kusaidiwa kutimiza ndoto zao.

Baada ya Fally kuiacha Quartier Latin International, ugomvi ulikuwa mkubwa zaidi baada ya taarifa zilizodai kuwa Koffi alikuwa akijaribu kuzuia albamu yake ya kwanza, ‘Droit Chemin’, isitoke.

Albamu hiyo iliweza kuingia sokoni na kuanzia hapo Fally Ipupa akawa msanii mkubwa kwenye kiwanda cha muziki nchini DRC, hali iliyozidisha uadui wake na Koffi.

Juni, 2026, kila mmoja kwa wakati wake alipokea mwaliko wa Rais Felix Tshisekedi lakini taarifa zinaeleza kuwa Koffi Olomide alikataa salamu ya Fally Ipupa walipokutana ndani ya Ikulu ya DRC.

Hata hivyo, miezi michache baaadaye, wawili hao walionekana kumaliza ‘bifu’ lao kwani Fally Ipupa alimtaja Koffi Olomide kwenye orodha ya wanamuziki ambao angewaweka kwenye ‘bendi bora ya DRC’. Koffi alipoona, akasema Fally Ipupa ni kipaji kikubwa katika ardhi ya nchi hiyo.

Tukija kwa Ferre Gola, bifu lake na Koffi lilianzia katika Bendi ya Quartier Latin International aliyojiunga nayo mwaka 2005 akitokea Wenge Musica Maison Mere iliyokuwa chini ya vichwa vitatu; Werrason, Didier Masela na Elongo Lodi.

Ferre Gola alisajiliwa na Quartier Latin International kwa dau la Dola za Marekani 20,000, ambacho kilikuwa kiasi kikubwa cha fedha wakati huo, na kusaini mkataba wa miaka miwili.

Licha ya kufanya vizuri kupitia nyimbo kama ‘Sisi Silivi’ na albamu ya ‘Danger de Mort’, Gola alisimamishwa kazi kwa muda kutokana na kile kilichoelezwa kuwa tabia ya utoro.

Mwishowe, Ferre Gola aliondoka kwenye Bendi hiyo mwaka 2006 akidai kuwa Koffi na uongozi mzima wa Bendi ya Quartier Latin International ulishindwa kuheshimu makubaliano ya awali.

Badala ya miaka miwili kama ilivyosainiwa kwenye mkataba, Ferre Gola alidumu mwaka mmoja tu, kisha akaianza safari akiwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Mwaka 2017, Koffi alimfungulia kesi Ferre Gola akidai kumchafua, kumtukana na kuvunja mkataba waliosaini mwaka 2005. Hiyo ilisababisha Ferre Gola kukamatwa na polisi, ingawa aliachiliwa baadaye.

Kwa sasa, hakuna taarifa rasmi kuthibitisha kuwa Koffi na Ferre Gola wamemaliza tofauti zao. Mwaka 2026, Koffi alipoulizwa nani mkali kati ya Fally Ipupa na Ferre Gola, alijibu wote.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles