14.4 C
New York

Tanesco yatwaa tuzo nne za mawasiliano

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetwaa tuzo nne katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), zikitambua ubora wake katika mawasiliano ya kimkakati, utoaji wa taarifa kwa umma na ubunifu katika kuelimisha wananchi.

Tuzo hizo zimetolewa Oktoba 8, 2026, ambapo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Lazaro Twange, amesema mafanikio hayo ni chachu ya kuendelea kuboresha mawasiliano na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma.

Gowelle amesema Tanesco itaendelea kutumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati na kwa njia rahisi na yenye ufanisi.

Ameishukuru PRST kwa kutambua mchango wa Shirika hilo, akisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Wizara ya Nishati, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Tanesco.

Pia, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika sekta ya umeme, unaosaidia kuimarisha miundombinu na matumizi ya teknolojia katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Savera Kazaura, aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, ameipongeza Tanesco kwa hatua iliyopiga katika kuboresha utoaji wa taarifa, hususan wakati wa changamoto za huduma ya umeme.

Kazaura amesema taasisi za umma zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mawasiliano ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na jamii.

Katika tuzo hizo, Tanesco imepata Tuzo ya Ubora katika Usimamizi wa Mawasiliano Wakati wa Migogoro (Crisis Communication Management), Tuzo ya Ubora katika Kampeni ya Elimu kwa Umma (Public Awareness Campaign) kupitia kampeni ya Nishati Safi ya Pika kwa Umeme, na Tuzo ya Idara Bora ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (Best Public Relations Department).

Tuzo ya nne imetolewa kwa Gowelle, aliyetangazwa Mtaalamu Bora wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Tanzania kwa mwaka 2026 (Best PR Practitioner 2026).

Tuzo za PRST hutolewa kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa mawasiliano katika kuimarisha sekta mbalimbali na kuongeza tija kwa wataalamu wa mawasiliano nchini.

Related articles

Recent articles