20.9 C
New York

Usajili umefungwa, simu za ‘mafundi’ hawa hazijaita

Published:

LONDON, Uingereza

USAJILI wa dirisha kubwa barani Ulaya ulifungwa rasmi juzi, Septemba 1, 2026, huku baadhi ya wanasoka wenye majina makubwa wakibaki hawana klabu za kucheza. Wako huru.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria, wachezaji hao wanaruhusiwa kujiunga na timu yoyote, hata kipindi hiki dirisha la usajili likiwa haliko wazi.

PAUL POGBA

Akiwa na umri wa miaka 33, kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa hana timu. Alijiunga na Monaco mwaka jana lakini ameachana nayo hivi karibuni akiwa amecheza mechi sita pekee. Majeraha ndiyo shida yake kubwa.

KARIM BENZEMA

Umri wake ni miaka 38. Aliondoka Real Madrid mwaka 2023 na kujiunga na Al Ittihad ya Saudia. Kwa miezi sita ya hivi karibuni alicheza Al-Hilal ya huko huko lakini sasa imemvunjia mkataba baada ya kuwasajili Crysencio Summerville, Ollie Watkins na Gabriel Martinelli.

RIYAD MAHREZ

Winga huyo raia wa Algeria ana umri wa miaka 35. Baada ya miaka mitatu ya kuitumikia Al Ahli, akiifungia mabao 37 katika mechi 122, amevunjiwa mkataba na klabu hiyo. Zipo taarifa kuwa anawindwa na Al-Shabab, ambayo pia inashiriki Ligi Kuu ya Saudia.

RAHEEM STERLING

Baada ya miezi mitatu tangu asajiliwe, Sterling ameachwa na klabu ya Feyenoord ya Uholanzi. Nje ya uwanja, anasubiri kesi yake ya kuendesha gari hovyo itakayosomwa mwezi ujao [Oktoba, 2026]. Je, ni klabu ipi itakayomsajili nyota huyo kipindi hiki?

PHILIPPE COUTINHO

Kiungo wa zamai wa Liverpool na Barcelona, Coutinho, aliachana na klabu ya Vasco de Gama tangu Februari, 2026. Alidai kuwa amechoka kiakili, lakini bado Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 34 hajatangaza rasni kuachana na soka.

JADON SANCHO

Mambo hayajawahi kukaa sawa kwake tangu alipojiunga na Manchester United mwaka 2021 akitokea Borussia Dortmund, usajili wake ukigharimu Pauni milioni 73. Ameondoka Old Trafford na huenda akajiunga na Palmeiras ya Brazil.

DANI CARVAJAL

Beki wa kulia huyo ana umri wa miaka 34. Ameondoka Real Madrid tangu Juni, 2026 baada ya kucheza mechi 451 kwa miaka 13 akiwa na timu hiyo. Bado haijafahamika ataibukia wapi, ikielezwa kuwa anatakiwa Saudia na Marekani.

JAMIE VARDY

Vardy [39], alimaliza msimu uliopita akiwa Cremonese ya Italia baada ya miaka 13 ya kucheza Leicester City. Ameondoka Cremonese baada ya timu hiyo kushuka Daraja. Zipo taarifa kuwa anawindwa na Wrexham, Sheffield Wednesday na West Ham za England.

DAVID ALABA

Umri wake ni miaka 34 na anafahamika kwa mafanikio yake ya kubeba mataji 12 ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika maisha yake ya soka. Beki huyo wa kulia aliondoka Madrid miezi minne iliyopita na hadi sasa hajasaini kokote.

SERGIO RAMOS

Umri ni miaka 40 na klabu yake ya mwisho kucheza ni Monterrey ya Mexico aliyoachana nayo Desemba, 2025. Mhispania huyo aliyepata mafanikio makubwa akiwa beki na nahodha wa Madrid, amejaribu mara kadhaa kununua hisa katika klabu ya Sevilla, ambayo ndiyo iliyoibua kipaji chake.

Related articles

Recent articles