24 C
New York

Msigwa atoa onyo kutumia vibaya vitambulisho vya NIDA

Published:

Na Esther Mnyika, Gazetini

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewaonya wananchi dhidi ya kukabidhi vitambulisho au namba zao za Taifa kwa watu wengine kwa ajili ya kusajili laini za simu, akisema matumizi hayo yanaweza kuwaweka wamiliki wa vitambulisho katika matatizo ya kisheria endapo namba hizo zitatumika kufanya uhalifu.

Msigwa ametoa onyo hilo leo, Septemba 1, 2026, wakati akitangaza kuanza rasmi kwa kampeni ya kitaifa ya “Septemba ya Utambulisho”, inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa utambulisho na matumizi sahihi ya huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vitambulisho vya ndugu au marafiki kusajili laini za simu, hali ambayo inaweza kusababisha mwenye kitambulisho kuwajibishwa kisheria iwapo laini iliyosajiliwa kwa taarifa zake itatumika katika uhalifu.

“Matumizi haya ya kutumia kitambulisho cha Taifa cha mtu yanaweza kumwingiza mwenye kitambulisho katika matatizo ya kisheria endapo laini hiyo itatumika kufanya uhalifu,” amesema Msigwa.

Amesema maendeleo ya teknolojia na kuunganishwa kwa mifumo ya Serikali yameongeza uwezo wa vyombo vya dola na taasisi nyingine kubaini na kufuatilia matumizi ya taarifa za utambulisho katika shughuli mbalimbali.

Vitambulisho milioni 1.5 bado

Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka wananchi ambao wamepata taarifa kwamba vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika kwenda kuvichukua katika ofisi za NIDA, akisema hadi sasa zaidi ya vitambulisho milioni 1.5 vilivyokamilika bado havijachukuliwa.

Amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika uzalishaji wa vitambulisho hivyo, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua hatua ya kuvifuata mara wanapopata taarifa kuwa vimekamilika.

“Wananchi waliopokea ujumbe wa simu unaowaarifu kuwa vitambulisho vyao vimekamilika kwenda kuvichukua katika ofisi za NIDA zilizopo wilayani Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, NIDA imeendelea kupanua usajili na utambuzi wa wananchi. Hadi Julai 2022, jumla ya watu 27,458,832 walikuwa wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.26 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

Katika kipindi hicho, vitambulisho 21,526,585 vilikuwa vimezalishwa, huku zaidi ya milioni 20 kati yake vikiwa tayari vimegawiwa kwa wananchi.

Taasisi 157 zaunganishwa

Msigwa amesema umuhimu wa mfumo wa utambulisho umeongezeka kutokana na hatua ya kuunganisha mifumo ya Serikali na sekta binafsi, hatua inayowezesha taasisi kuhakiki taarifa za watu wanaotafuta huduma.

Amesema hadi Agosti 2026, jumla ya taasisi 157, zikiwemo taasisi 72 za Serikali na 85 za sekta binafsi, zilikuwa zimeunganishwa na mfumo wa NIDA.

Kwa mujibu wa Msigwa, mfumo huo unasaidia taasisi kuhakiki taarifa za watu wanaopata huduma na kupunguza uwezekano wa udanganyifu pamoja na matumizi ya taarifa zisizo sahihi.

“Mfumo huo unasaidia taasisi kuhakiki taarifa za watu wanaopata huduma na kupunguza uwezekano wa udanganyifu na matumizi ya taarifa zisizo sahihi,” amesema.

NIDA kuboresha teknolojia

Aidha, Msigwa amesema Serikali imeanza kuboresha teknolojia inayotumika katika uchapishaji wa vitambulisho vya Taifa kwa lengo la kuongeza uimara wa kadi hizo pamoja na usalama wa taarifa zilizomo.

Amesema Serikali pia inapanga kuwa na kadi zenye uwezo mkubwa zaidi wa kubeba taarifa za utambulisho zinazohusiana na huduma nyingine, hatua ambayo inalenga kupunguza idadi ya vitambulisho ambavyo wananchi hulazimika kubeba wanapohitaji huduma mbalimbali.

Kwa upande mwingine, NIDA itaendelea kuboresha teknolojia ya utambuzi wa kibaiolojia kwa kutumia sura na mboni za macho ili kuongeza uwezo wa kuwatambua watu ambao alama zao za vidole haziwezi kutumika kwa ufanisi.

Kampeni ya “Septemba ya Utambulisho” itafikia kilele Septemba 16, 2026, ikiwa ni Siku ya Utambulisho Duniani, huku shughuli za uhamasishaji, utoaji wa elimu na huduma za NIDA zikiendelea nchini kote hadi Septemba 30.

Msigwa amewataka Watanzania, taasisi za umma, sekta binafsi na vyombo vya habari kutumia mwezi huo kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa utambulisho na matumizi sahihi ya vitambulisho vya Taifa.

Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Kipo, Chukua, Kamilisha safari yako.”

Amesisitiza kuwa utambulisho hauishii kwenye kuwa na kadi ya Taifa pekee, bali ni msingi muhimu wa upatikanaji wa huduma, usalama, ujenzi wa uchumi wa kidijitali na maendeleo ya taifa.

Related articles

Recent articles