21.7 C
New York

Nchi zenye ‘sura ya ugaidi’ mbele ya Marekani

Published:

LOS ANGELES, Marekani

MAREKANI imeiondoa Syria katika orodha ya nchi inazoamini zinafadhili vitendo vya kigaidi (SSOT). Hatua hiyo ni mwendelezo wa uhusiano mzuri wa mataifa hayo tangu kuanguka kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad nchini humo.

Kama itakumbukwa, Al-Assad aliondoshwa madarakani Desemba, 2024, baada ya miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na hivi karibuni alihukumiwa kifo akiwa nje ya nchi hiyo tangu alipokimbia baada ya utawala wake kuangushwa.

Akipokea kwa furaha taarifa ya Marekani kuwaondoa kwenye listi ya nchi zinazofadhili ugaidi, Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, amesema ni hatua muhimu inayoonesha ustawi wa Taifa hilo la Kiarabu.

Serikali ya Marekani imeeleza kuridhishwa na ushirikiano inaoupata kutoka kwa utawala wa Al-Sharaa, hasa katika harakati za kulimaliza Kundi maarufu la kigaidi la ISIL (ISIS).

Kama itakumbukwa, Al-Sharaa aliwahi kuwa kiongozi wa Al-Nusra Front, moja ya makundi ya kigaidi yanayofanya kazi na Al-Qaeda, lakini aliachana nalo mwaka 2016.

Marekani imekuwa ikiitambua Syria kama nchi inayofadhili ugaidi tangu mwaka 1979, wakati huo Rais akiwa baba yake Al-Assad, Hafez, lakini Rais Donald Trump alitangaza Julai, 2026, kwamba wataiondosha kwenye listi hiyo.

Ifahamike, Marekani inapoiweka nchi kwenye orodha yake hiyo, ni kwamba itakuwa imeathiri ushawishi wake wa kupata misaada ya nje, kufanya baadhi ya miala ya kifedha, na hata kuogopwa na kampuni za nje zinazotaka kuwekeza.

Baada ya Syria ‘kuchomolewa’, inaziacha Cuba, Iran na Korea ya Kaskazini katika orodha hiyo ya ‘magaidi’ wa Marekani.

Iran imekuwa kwenye listi hiyo tangu mwaka 1984 baada ya jeshi la mapinduzi ya Kiislam kuingia madarakani. Madai ya Marekani ni kwamba mamlaka za Iran zimekuwa zikifadhili vikundi vya kigaidi ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Cuba imekuwa kwenye orodha hiyo tangu mapinduzi yam waka 1982. Marekani haikuridhishwa na kitendo cha Fidel Castro kuipindua Serikali iliyokuwa ikiongozwa na ‘kibaraka’ wao, Fulgencio Batista, mwaka 1959.

Wakati wa utawala wa Rais Barack Obama, Marekani, iliitoa Cuba kwenye listi hiyo lakini Rais wa sasa, Trump, aliirejesha mwishoni mwa awamu yake ya kwanza madarakani.

Korea ya Kaskazini ilianza kutambulika rasmi kama nchi inayofadhili ugaidi, kwa mujibu wa Marekani, mwaka 1988. Ni baada ya watu 115 kufariki katika tukio la ndege ya Korea kushambuliwa.

Mwaka 2008, Marekani iliiondoa Korea kwenye listi hiyo baada ya mazungumzo mazuri juu ya nyuklia, lakini Rais Trump aliirejesha katika awamu yake ya kwanza ya uongozi mwaka 2017.

Related articles

Recent articles