23.5 C
New York

Wananchi wanasemaje kuhusu JNHPP?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

NI safari ya miaka takribani saba, ikianza kama ndoto iliyobeba maono makubwa ya kuimarisha hali ya upatikaji wa huduma ya uhakika ya nishati ya umeme hapa nchini.

Safari ya uwekezaji wa Shilingi trilioni 7.452 za Tanzania iliyoanza Juni, 2019, ikisimamiwa na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) na Wizara ya Nishati, na sasa zimebaki siku chache tu kuanza kuona matunda yake.

Kwa ufupi, ni ndoto iliyotimia, ambapo uzinduzi rasmi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) utafanyika Agosti 22, 2026, katika eneo la mradi huko Rufiji, mkoani Pwani.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi wakati wa hafla hiyo, huku kukamilika kwa kituo hicho kukielezwa kuwa na tija kubwa katika uboreshaji wa upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme nchini.

Ndiyo, ni mradi unakwenda kuizalishia nchi Megawati 2,115, hivyo kuchangia takribani asilimia 45 kwenye Gridi ya Taifa.

Hivyo basi, JNHPP si tu unakuwa mradi mkubwa zaidi kuwahi kujengwa nchini, bali pia umefadhiliwa kwa asilimia kubwa kupitia mapato ya kodi za Watanzania.

Kwa upande mwingine, Bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo bilioni 33 za maji, likiwa na ukubwa wa mara 10 zaidi ya Bwawa la Mtera.

GAZETINI kwa nyakati tofauti imezungumza na baadhi ya Watanzania kuhusu umuhimu wa bwawa hilo linalotarajiwa kuzinduliwa Agosti 22, 2026. Miongoni mwao ni Damas Mkinga, mkazi wa Rufiji, Pwani, anasema mradi huo umekuwa na faida hata kabla ya kukamilika kwake.

“Niseme tu, kwamba mradi huu umekuwa na faida kubwa tangu ulipoanza mwaka 2019. Tumeshuhudia vijana wetu zaidi ya 10,000 wakipata ajira katika ngazi tofauti,” amesema Damas.

“Pia, kwa upande wangu, faida nyingine ninavyoweza kuiona ni hii ya kudhibiti mafuriko Bonde la Rufiji na hata kutuboreshea kilimo cha umwagiliaji.”

Kwa upande wake, Martha Mjaka, mkazi wa Wilaya ya Bagamoyo, Pwani, anasema JNHPP ni mfano halisi wa namna Tanzania inayoweza kutekeleza miradi yake ya kimkakati pasi na kutegemea nguvu kubwa ya misaada ya nje.

“Ni jambo zuri kuona miradi ya aina hii inatekelezwa kwa kutegemea sehemu kubwa ya mapato ya ndani. Miradi ya namna hii haiachi makovu ya madeni ya nje. Niipongeze Serikali katika hilo.

“Hii ina maana gani? Tanzania iko vizuri kiuchumi, kiasi cha kumudu miradi mikubwa pasi na kusubiri fedha za wahisani. Kwa mtazamo wangu, hii ni hatua kubwa kwa uchumi wa nchi,” amesema Martha.

Naye Bonita Mwila, mkazi wa Kibaha, Pwani, anasema ongezeko la Megawati zaidi ya 2,000 linakwenda kugusa maisha ya wananchi, hasa wa kipato cha chini.

“Vilevile, kama tulivyoona, zinakwenda kuongezeka Megawati zaidi ya 2,000. Hii inamaanisha upatikanaji wa umeme unakwenda kuwa wa uhakika zaidi.

“Tunakwenda kuepukana na adha ya umeme kukatika mara kwa mara, changamoto ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi kwetu sisi wananchi, hasa wa kipato cha chini.”

Aidha, mbali na faida hizo, kuwa na umeme wa uhakika baada ya kukamilika kwa JNHPP kunatarajiwa  kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii.

Rogers Kasha, mkazi wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, anaiona hiyo ikiwa na tija kubwa katika ustawi wa kijamii na kiuchumi.

“Mradi huu utasiaida kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati kutoka nje, yakiwamo mafuta, ambayo tunaweza kuwa tunanunua kwa bei kubwa,” amesema.

Related articles

Recent articles