Na mwandishi wetu, Gazetini
ANAREJEA! Hatimaye klabu ya Yanga inatarajiwa kumtambulisha kiungo raia wa Burkina Faso, Stephanie Azizi Ki, ifikapo kesho Agosti 15, 2026.
Kwa miezi kadhaa sasa, Aziz Ki aliyeondoka Yanga mwaka 2025 na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco amekuwa akihusishwa na mpango wa kurudi Jangwani.
Yanga, kwa upande wao, wamethibitisha kuwa kesho watamtangaza mchezaji mpya wa kigeni na taarifa za uhakika ambazo GAZETINI imezinasa zimedai kuwa si mwingine, bali ni Aziz Ki.
Gazetini inafahamu kuwa Yanga, licha ya usajili mkubwa iliofanya kipindi hiki cha dirisha kubwa, bado inahitaji mtu mpya kwenye eneo la kiungo mshambuliaji (namba 10).
Awali, duru za usajili zilidai kuwa Yanga ilikuwa kwenye harakati za kumnasa kiungo wake mwingine wa zamani, Feisal Salum ‘Fei Toto’ lakini dili hilo limeota mbawa.
Aidha, taarifa ambazo Gazetini ina uhakika nazo zinadai kuwa biashara ya Fei Toto imekuwa ngumu kutokana na dau kubwa la kuvunja mkataba wake na matajiri wa Chamazi.


