27.2 C
New York

Bashar al-Assad: Rais ‘dikteta’ aliyeangukia hukumu ya kifo (3)

Published:

DAMASCUS, Syria

KATIKA sera za mambo ya nje, utawala wa Assad haukuwa na tofauti yoyote na ule wa baba yake. Kama alivyokuwa baba, naye aliendeleza uhusiano mbaya na Marekani, Israel na mataifa ya Ulaya Magharibi.

Assad alisisitiza mara kadhaa kupitia hotuba zake, kwamba Syria haiwezi kuwa rafiki wa Israel hadi pale Taifa hilo litakaporesha ardhi yake iliyochukua tangu mwaka 1967.

Wakati huo huo, Assad hakuficha kuwa Serikali yake iko upande wa Palestina katika mgogoro wao na Israel huko Gaza.

Kama itakumbukwa, pia Assad haukuwa rafiki wa Marekani. Alikosoa hatua ya Taifa hilo kubwa kuivamia kijeshi Iraq mwaka 2003.

Miaka miwili baadaye, Marekani iliishitumu Syria kuhusika katika shambulizi la bomu mjini Beirut lililosababisha kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon, Rafik Hariri.

Wakati huo, kama itakumbukwa, Syria ilikuwa na wanajeshi wake huko Lebanon na tukio hilo lilisababisha waondolewa na kumalizika kwa vita iliyodumu miaka 29 kati ya mataifa hayo.

Kutokana na uhusiano mbaya kati yake na Marekani na Israel, Assad alilaumu mataifa ya nje baada ya kuibuka kwa maandamano makubwa ya raia nchini Syria mwaka 2011.

Assad alisema maandamano hayo ya kupinga utawala wake yaliyoanzia mjini Deraa, Kusini mwa Syria, yalitokana na magaidi wa ndani walioshawishiwa na nchi za nje.

Yalianza kama utani, kisha kuenea nchi nzima, ambapo wafuasi wa upinzani walifikia hatua ya kumiliki silaha na kupigana na vyombo vya dola, kwa maana ya polisi na wanajeshi.

Miezi michache baadaye, Serikali ya Assad ilijikuta kwenye wakati mgumu zaidi baada ya waasi kuteka maeneo mengi ya Kaskazini na Mashariki mwa nchi hiyo. 

Ni wakati huo pia, muungano wa upinzani, National Coalition, ukawa na nguvu kubwa na kutambuliwa na nchi zaidi ya 100 kama wawakilishi wa wananchi wa Syria.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2012, tayari watu zaidi ya 60,000 walishapotea maisha, huku Assad akisisitiza kuwa hawezi kukaa mezani na waasi kwani ni ‘maadui wa Mungu’ na ‘vibaraka wa mataifa ya Magharibi’.

Mwanzoni mwa mwaka 2013, vikosi vya jeshi na polisi vya Serikali viliweza kurejesha udhibiti wake katika miji ya Kusini na Magharibi iliyokuwa imetekwa na waaasi.

Kama itakumbukwa, mafanikio hayo yalitokana na nguvu waliyopewa na kundi la Hezbollah la Lebanon lililoingia Syria kumsaidia Assad.

Hata hivyo, ni wakati ambao Marekani, Ufaransa na Uingereza ziliwatupia lawama wapiganaji wa Serikali kwa madai kuwa walitumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake kwa raia mjini Damascus.

Wakati hali ikiwa imetulia kwa kiasi kidogo, Assad aligombea tena kiti cha urais na kushinda awamu yake ya tatu katika Uchaguzi wa mwaka 2014. Safari hii, alipata ushindi wa asilimia 88.7 ya kura.

Lakini, tatizo jipya kwa Serikali ya Assad likawa ni ujio wa kundi jipya la kigaidi, Islamic State (IS), ambalo mwaka 2015 lilifanikiwa kuteka Mji wa Idlib wa Kaskazini na maeneo mengine ya Mashariki mwa Syria.

Hiyo ilisababisha Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kuagiza wanajeshi wake kuingia Syria na kuisaidia Serikali ya Assad kukabiliana na kikundi hilo.

Urusi ilisema kuingia kwake Syria ni kwa lengo la kutokomeza magaidi wa IS, ingawa baadaye ililaumiwa kwa kushambulia makazi ya raia wasio na hatia katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Taarifa ya watetezi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN) ilieleza kuwa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu vya Serikali ya Assad na Urusi vilisababisha mamia ya watu kufariki na maelfu kukimbia makazi yao.

Usikose sehemu ya nne ya makala haya … Tembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles