Na mwandishi wetu, Gazetini
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC, wamekamilisha usajili wa winga wa kimataifa kutoka Zambia, Albert Kangwanda, kwa mkataba wa miaka miwili ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Kangwanda (27) ambaye amesaini mkataba usiku wa saa tano, Julai 24, 2026 mbele ya Rais wa Yanga Injinia Hersi Said, anatua Jangwani akitokea klabu ya Red Arrows ya Zambia, baada ya kujijengea uzoefu katika ligi mbalimbali barani Afrika na Ulaya.
Kabla ya kujiunga na Red Arrows, nyota huyo aliwahi kuichezea Al-Hilal Omdurman ya Sudan, CSF Spartanii ya Moldova na HNK Gorica ya Croatia.
Yanga inaamini uzoefu wa Kangwanda katika ligi tofauti utasaidia kuongeza ushindani kikosini na kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu wa 2026/27, ambapo klabu hiyo itashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa.


