19.4 C
New York

Meya wa New York arudi nyuma kumkamata Netanyahu

Published:

NEW YORK, Marekani

MEYA wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, amesema hana mamlaka ya kisheria ya kumkamata Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, iwapo atatembelea jiji hilo, akibadili msimamo wake wa awali uliokuwa umeibua mjadala mkubwa kisiasa na kisheria.

Kupitia video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mamdani alisema baada ya kufanya mashauriano na timu yake ya wanasheria, imebainika kuwa ofisi ya meya haina uwezo wa kutekeleza hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Badala yake, Mamdani ameutaka utawala wa Marekani kuchukua hatua kuhusu hati hiyo na kuzingatia kujiunga na ICC ili kuwezesha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hiyo.

Awali, katika mahojiano na gazeti la The New York Times, Mamdani alisema alikuwa akifanya mazungumzo na vyombo vya sheria kuhusu uwezekano wa kutekeleza hati hiyo endapo Netanyahu angewasili New York. Hata hivyo, alifafanua baadaye kuwa mamlaka ya kutekeleza hati za aina hiyo yako chini ya serikali ya shirikisho, si ofisi ya meya.

Kwa mujibu wa sheria za ICC, nchi wanachama wa mahakama hiyo zinapaswa kushirikiana katika utekelezaji wa hati za kukamatwa. Hata hivyo, Marekani si mwanachama wa ICC, hivyo haina wajibu wa kisheria wa kutekeleza hati zilizotolewa na mahakama hiyo.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesisitiza kuwa Netanyahu hatakamatwa akiwa nchini humo. Trump amesema utawala wake unaendelea kumuunga mkono kiongozi huyo wa Israel, akieleza kuwa anapambana na vitisho vya kiusalama vinavyoikabili Israel, ikiwemo Iran.

Kauli za Mamdani na Trump zimeibua mjadala mpya kuhusu mipaka ya mamlaka ya viongozi wa serikali za mitaa, nafasi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na utekelezaji wa sheria za kimataifa.

Related articles

Recent articles