Na Hassan Mwasha, Gazetini
YANGA wanaelekea katika Uchaguzi Mkuu, ambapo mchakato huo wa kidemokrasia unatarajiwa kufanyika Agosti 2, 2026.
Ukiwa ni mwezi mmoja kabla ya Uchaguzi, nafasi ya urais imeonekana kukosa ushindani baada ya Injinia Hersi Said kupitishwa kuwa mgombea pekee.
Kwamba kabla ya Uchaguzi, tayari Injinia Hersi ana uhakika wa kurudi madarakani hata kabla ya kupigiwa kura.
Swali la msingi; unafikiri hakuna wanachama wa Yanga wanaotamani kiti cha urais? Wapo, tena huenda ni wengi mno. Si dhambi.
Ila sasa, kwa jicho la kawaida, Injinia Hersi ‘ameua’ ushindani kwenye nafasi aliyopo. Kwa ufupi, amezima ndoto za wanaotamani kukalia kiti chake.
Na kwa namna hali ilivyo, huenda ndoto walizonazo zikachukua muda mrefu kutimia au zisitimie kabisa.
Ieleweke kwamba Injinia Hersi halazimishi kubaki kwenye kiti, bali analindwa na kile alichoifanyia Yanga katika muhula wake wa kwanza ulioanza mwaka 2022.
Ukweli ulio wazi ni kwamba chini ya uongozi wake, Yanga imekuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja. Nani mwenye akili timamu atapingana na uhalisia huo?
Ukivuta picha alivyoikuta Yanga miaka minne iliyopita, utakubaliana na mimi kwamba ni ‘dhambi ya soka’ si tu kumpinga, bali hata kuitaka kofia yake kwa kipindi hiki.
Huwezi kueleweka si tu kwa mashabiki na wanachama wa Yanga, bali hata kwa kila aliyeshuhudia miaka minne ya utawala wa Injinia ndani ya Yanga.
Kiumbe ambaye aliikuta Yanga ikiwa taabani ndani na nje ya uwanja. Ikiwa dhohofu kiushindani wa mataji na hata kiuchumi.
Yanga ambayo msamiati wa umoja na mshikamano ulifunikwa na migogoro isiyokwisha. Yanga iliyopasuka kwa mivutano ya makundi ndani ya klabu.
Ukitafakari yote hayo, kisha ukatazama muda mfupi aliokaa madarani, inakuhitaji ujasiri wa hali ya juu hata kunong’ona, achilia mbali kusema hadharani kuwa unautaka urais wa Yanga kipindi hiki.
Historia inakumbusha, kwamba watu waliojaribu kukosoa au kuja na mawanzo kinzani dhidi ya uongozi wa Injinia Hersi hawakubaki salama.
Bila hata Injinia Hersi kunyanyua mdomo kuwajibu, watu wa aina hiyo walishughulikiwa na mashabiki na wanachama wenzao.
Waligeuka ‘maadui’ na kukatwa juu kwa juu na wenzao wanaotambua, kuheshimu na kuthamini mchango mkubwa wa Injinia ndani ya Yanga.
Kama walinusurika sana, basi waliishia kutukanwa, kuitwa ‘chawa’, wasaliti na wasioitakia mema klabu ya hiyo.
Kwamba kwa mashabiki na wanachama walio wengi, Injinia Hersi ni ‘untouchable’ (asiyegusika) ndani ya klabu.
Katika mazingira ya aina hiyo, unawezaje kusimama hadharani na kusema inataka kugombea dhidi ya mtu wa aina hiyo?
Kinyume chake, unapaswa kutulia, kuficha dhamira yako na kusubiri wakati sahihi uamue hatima ya Injinia Hersi ndani ya Yanga.
Ni upi wakati sahihi? Ni swali gumu. Jibu rahisi ni hili; Injinia atakapoamua kukaa kando au mashabiki na wanachama wa Yanga watakapoona hafai tena kuiongoza klabu yao.


