27 C
New York

Urafiki uliogeuka uadui Trump, Waziri Mkuu wa Italia

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

UHUSIANO kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, umeendelea kuwa gumzo na hata kuibua mjadala wa aina yake kwenye duru za kisiasa ulimwenguni.

Trump na Meloni walikuwa marafiki wakubwa katika miaka ya hivi karibuni, kabla ya kugeuka ‘chui na paka’ kuanzia mwaka 2025.

Wakati huo, wengi walimwita Meloni kuwa ni ‘mpambe’ wa Trump kwa namna wawili hao walivyokuwa na ukaribu mkubwa.

Kama itakumbukwa, Waziri Mkuu huyo wa Italia alikuwa kiongozi pekee kutoka nchi za Jumuhiya ya Ulaya (EU) aliyepewa siti za mbele katika hafla ya kuapishwa kwa Trump (Januari, 2025).

Miezi mitatu baadaye, kutokana na uhusiano wake mzuri na Rais Trump, Meloni alichaguliwa kuongoza msafara wakati viongozi wa EU walioitembelea Ikulu ya Marekani.

Kama itakumbukwa, ziara hiyo ililenga kuzungumza na Trump juu ya hatua ya kiongozi huyo kuziwekea tozo kubwa bidhaa zinazotoka katika Jumuhiya hiyo.

Hata hivyo, kile kilichoonekana kuwa ni mwanzo wa uadui, Wizara ya Ulinzi ya Italia iligoma kuiruhusu Marekani kutumia ardhi yake kama kambi ya kijeshi katika vita vyake na Iran.

Hiyo ilikuwa Machi, 2026, ambapo hatua hiyo ilitokana na msimamo wa miaka mingi na wa kikatiba wa Italia kujiweka mbali na masuala ya vita.

Wiki chache tu baadaye, Trump alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Truth Social kumshambulia kwa maneno kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV.

Hilo halikuifurahisha Serikali ya Italia, nchi yenye ufuasi mkubwa wa Katoliki, hivyo Meloni kumjibu Trump akisema kauli zake dhidi ya Papa Leo hazikubaliki.

Kauli hiyo haikumfurahisha Trump, hivyo kujibu: ” (Meloni) amenishanga. Hakubaliki. Amebadilika, hata Italia haiko kama ilivyokuwa.”

Wiki chache zilizopita, ilionekana kama wawili hao wamemaliza tofauti zao. Ni baada ya picha ya pamoja iliyowaonesha wakiwa kwenye Mkutano wa G7 iliyofanyika mjini Évian-les-Bains, Ufaransa.

Katika picha hiyo, Trump na Meloni walionekana wakiwa wamezama kwenye maongezi, na bibiye huyo alikuja baadaye na kusema hakuna uadui kati yao.

Hata hivyo, siku chache baadaye, iliibuka tena tofauti kati yao baada ya Trump kukiambia kituo cha televisheni cha Italia, La7, kwamba Meloni ndiye aliyemuomba wapige picha.

Trump alidai kuwa Meloni alimbembeleza wapige picha, ikiwa ni katika kujipendekeza baada ya kuona Marekani imeshinda vita vyake dhidi ya Iran.

“Aling’ang’ania kupiga picha na mimi. Sikutaka, ila nilimuonea huruma,” alisema Trump akiiambia La7.

Meloni hakusubiri lipoe. Naye aliposti video kumjibu Trump, akisema Rais huyo ameamua kudanganya.

“Sijui kwanini Rais wa Marekani anakuwa na tabia hizi kwa washirika wake,” alisema Meloni na kuongeza: “Inasikitisha kuona Trump hafanyi hivyo dhidi ya maadui wa nchi za Magharibi.”

Bi Meloni alisisitiza kuwa sisi yeye wala Italia waliomuomba Rais Trump kupiga picha wakati wa Mkutano wa G7 nchini Ufaransa.

Pia, Rais wa Italia, Sergio Mattarella, alimpigia simu Meloni na kumpoza kwa tukio hilo, huku Bunge likilaani kwa kusema kilichotokea ni udhalilishaji dhidi ya nchi yao.

Ni baada ya mzozo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, alisitisha ziara yake mjini Washington, Marekani.

Related articles

Recent articles