27.9 C
New York

Mabeberu, majirani wanavyopishana ‘kuchota utajiri’ wa DRC

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAKATI wengine wakiamini DRC imefeli katika diplomasia na ulinzi, vita vinavyoendelea nchini humo vinahusishwa pia na hila za mataifa makubwa duniani.

Kwamba yamekuwa chanzo cha migogoro isiyokwisha katika nchi hiyo kwa lengo la kuifarakanisha ili yatumie nafasi hiyo kuchota utajiri wa madini.

Kwa miaka mingi, mikoa ya Mashariki mwa DRC, ambako ndiko uliko utajiri wa madini uliko imekuwa kwenye machafuko yanayoongozwa na M23.

Unazungumzia madini ya aina tatu yenye thamani kubwa, yakihitajika zaidi katika maendeleo ya teknokojia ya karne hii ya 21; cobalt, colta na dhahabu.

Mathalan, DRC ina akiba ya asilimia zaidi ya 70 ya madini ya cobalt, ambayo hutumika kutengeneza simu-janja na magari ya umeme.

Wakati huo huo, DRC inamiliki asilimia 80 ya akiba ya coltan duniani, madini ambayo muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya umeme.

Mataifa ya Magharibi, sambamba na majirani wa DRC – Rwanda na Uganda – yanatajwa kunufaika na uasi wa Kundi la M23, ambalo sasa linashikilia maeneo mengi ya Mashariki, ikiwamo Miji ya Walikale, Goma na Bukavu.

RWANDA

Ni kwa miaka mingi, Marekani na Ufaransa, pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), I zimekuwa zikishutumu Serikali ya Rwanda kwa kuisaidia M23 na vikundi vingine vya waasi.

Aidha, ripoti zinaeleza kuwa sehemu kubwa ya madili yanayoibiwa DRC na kupelekwa katika soko la kimataifa hupitia Rwanda.

Vilevile, licha ya kiwango kidogo ilichonacho Rwanda katika akiba ya dhahabu, imekuwa ikiuza madini hayo kwa wingi, ikitafsiriwa kuwa inaiba kutoka DRC.

Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi, Rwanda kupitia operesheni za kijeshi, imekuwa ikiwaibia DRC madini ya cobalt na colta na kuvuna fedha nyingi.

UGANDA
Vikosi vya Uganda viko Mashariki mwa DRC, vikiripotiwa kuwasaidia kwa karibu waasi wa M23. Ni mwendelezo wa kile kilichoanza tangu mwaka 1998.

Kwa mujibu wa Uganda, wako hapo kwa ajili ya kupigana na vikundi vya kigaidi, wakiwamo Allied Democratic Forces (ADF) lakini ripoti zinadai kuwa kuna ajenda nyingine ya wizi wa rasilimali za DRC.

Mwaka 2017, Uganda ilishangaza wengi, hata jumuhiya za kimataifa, baada ya kusafirisha madini ya dhahabu yenye thamani ya Dola milioni 377.

Kwa mujibu wa habari za kiuchunguzi, Uganda iliiba sehemu kubwa ya madili hayo kutoka katika mgongo wa ardhi ya majirani zao (DRC).

URUSI

Licha ya kwamba haiko mstari wa mbele kama zilivyo Rwanda na Uganda, Urusi nayo imejipenyeza na kupata nafasi katika mgogoro wa DRC.

Mwaka 2021, katika kile kilichoonekana ni msaada wa kiusalama, iliipatia Serikali ya DRC silaha za kukabiliana na waasi. Bunduki 10,000 na mabomu yenye thamani ya euro milioni 3.

Baadaye, mwanadiplomasia wa Urusi, Viktor Tokmakov, alifanya ziara mjini Kinshasa, na kuahidi ujenzi wa kambi yao ya kijeshi nchini DRC.

Hata hivyo, zipo ripoti zinazoeleza kuwa ushirikiano huo umekuwa na faida kwa Urusi, huku ukiigharimu DRC kiwango kikubwa cha madini Kama sehemu ya ‘kulipa fadhila’.

CHINA

Iko wazi kuwa kampuni mbalimbali kutoka katika Taifa hilo ziko DRC zikitawala vilivyo kwenye uchimbaji, uchenjuaji na usafirishaji wa madini.

Takwimu pia zinathibitisha hilo zikionesha China kumiliki asilimia 60 ya uzalishaji wa cobalt nchini DRC.

Mbali ya kuibiwa rasilimali zao, raia wa DRC katika maeneo ya migodi, hasa Miji ya Kolwezi na Lubumbashi, wamekuwa wakipitia mateso makali na ya aina yake.

Ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International ilithibitisha hilo, ikionesha kuwa raia wamekuwa wakitekwa, wakibakwa na hata kulazimishwa kuyahama makazi yao.

Related articles

Recent articles