24.5 C
New York

Mjamzito anusurika kuuawa na tembo

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini- Serengeti

MWANAMKE mmoja mjamzito, Bhoke Mahumo (28), mkazi wa Kijiji cha Mbirikili, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, amenusurika kufa baada ya kukutana uso kwa uso na tembo ambaye alimshika kwa mkonga na kumfukia ndani ya shimo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, William Mugaya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Juni 13, mwaka huu, majira ya saa 2:00 asubuhi katika Kitongoji cha Senta kijijini hapo.

Mugaya amesema mwanamke huyo alikuwa anatoka dukani kununua dawa majira ya asubuhi na alipofika eneo hilo ghafla alikutana uso kwa uso na tembo huyo aliyekuwa akitokea maeneo ya Gereza la Tabora B.

Mwenyekiti huyo amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, aliwataka wananchi waliokuwa karibu na eneo la tukio kumchukua mwanamke huyo na kumpeleka Hospitali ya Nyerere DDH kwa matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake. Taarifa hizo pia zimethibitishwa na Diwani wa Kata ya Sedeco, Raphael Matiko.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere DDH, Dkt. Tanu Waryoba, amesema walimpokea mwanamke huyo Juni 13 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi akiwa amepoteza fahamu. Baada ya kufanyiwa uchunguzi, madaktari walibaini alikuwa na maumivu makali ya kifua pamoja na michubuko katika sehemu mbalimbali za mwili, hususan usoni na miguuni. Aidha, alibainika kuwa ni mjamzito wa miezi minane.

“Hali ya mwanamke huyo inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu, ingawa bado analalamika maumivu ya kifua. Tutamfanyia uchunguzi zaidi kwa kutumia X-ray katika eneo hilo pamoja na mbavu,” amesema Dkt. Waryoba.

Akizungumza na mwandishi wa habari akiwa katika Wodi ya Wajawazito ya Hospitali ya Nyerere DDH, Bhoke Mahumo alisimulia mkasa huo akisema alitoka nyumbani kwenda dukani kununua dawa za maumivu kwa mume wake, Joseph Nyakitimo.

Alisema akiwa njiani kurejea nyumbani, katikati ya makazi ya watu, ghafla alikutana na tembo uso kwa uso.

“Nilisimama nikavua viatu, tembo naye akasimama. Tukawa tunaangaliana uso kwa uso. Nikamuomba msamaha, akanyanyua mkonga na kusimamisha masikio kutafuta upepo. Nikaamua kukimbia, lakini tembo akaanza kunikimbiza huku akipiga kelele. Nilipokaribia kuingia katika kaya ya Chacha Masero, nilihisi tembo huyo ananishika kwa nguvu kwa mkonga wake na kunivuta pembeni,” amesema Mahumo.

Amesema baada ya kumvuta pembeni, tembo huyo alianza kuchimba shimo. Baada ya kumaliza, alimweka katikati ya miguu yake, akamlaza ndani ya shimo na kuanza kumfukia kwa udongo.

“Baada ya kumaliza kunifukia, tembo huyo alinikojolea juu ya shimo. Mkojo huo ulisababisha mwili wangu kuwasha,” amesema.

Mahumo amesema akiwa ndani ya shimo na tayari amefukiwa, alisikia sauti za wananchi wakisema tembo huyo ameondoka ndipo alipoanza kuomba msaada.

“Nilitoa sauti na kujaribu kuondoa udongo sehemu ya kifua. Alifika mke wa Chacha Masero aitwaye Nchagwa Masero ambaye alijaribu kunitoa lakini alishindwa. Akaenda kumuita mume wake ambaye alifika na kufanikiwa kunitoa ndani ya shimo. Baadaye walimjulisha mume wangu ambaye alifika na kunipeleka hospitali ambako bado ninaendelea na matibabu,” amesema.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Kitongoji cha Shuleni, Chacha Itembe (47), amesema wanyama aina ya fisi walivamia nyumba yake inayotumika kuhifadhi mbuzi na kondoo usiku wa kuamkia Juni 14 mwaka huu na kuua kondoo wanne pamoja na mbuzi mmoja.

Akizungumza na Gazetini, Itembe amesema zaidi ya fisi 10 walivamia kaya yake wakati familia ikiwa imelala, wakachimba ukuta wa banda la mifugo na kuingia ndani.

Amesema aliyegundua tukio hilo ni mke wake, Sabina Mkami, ambaye alimwamsha saa 11 alfajiri baada ya kuona mifugo hiyo imeuawa.

Itembe amesema mifugo hiyo ilikuwa na thamani ya Shilingi 900,000, ambapo kila kondoo alikuwa na thamani ya Shilingi 200,000 na mbuzi mmoja Shilingi 100,000.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Shuleni, Ryoba Muhere, amethibitisha tukio hilo na kusema ni mara ya pili kwa fisi kuvamia kaya ya Itembe na kuua mifugo yake. Amesema kutokana na tukio hilo, Itembe amebaki bila mbuzi wala kondoo.

Related articles

Recent articles