JERUSALEM, Israel
WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, atawania tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao, Chama chake cha Likud kimeeleza.
Kwamba mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 76, ambaye ameiongoza Israel tangu mwaka 2009, atawania kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2026.
“Waziri Mkuu Netanyahu atagombea katika Uchaguzi Mkuu ujao na atashinda,” imeeleza taarifa ya Chama hicho juzi Juni 10, 2026.
Taarifa ya Chama cha Likud imekuja zikiwa ni siku chache tu zimepita tangu Rais wa Marekani, Donald Trump, aliposema haoni kama Netanyahu ataendelea na siasa.
Rais Trump alisema hayo wakati huu Marekani ikiripotiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na Israel, ambao ni washirika wao wakubwa kwa miaka mingi.
Netanyahu, ambaye ndiye Waziri Mkuu aliyedumu madarakani kwa muda mrefu zaidi katika historia ya siasa za Israel, kwa sasa anakabiliwa na mashitaka ya rushwa.
Wakati huo huo, taswira yake imechafuliwa na miaka mitatu ya nchi hiyo kuingia kwenye vita. Ni pamoja na vita dhidi ya wapiganaji wa Hezbollah huko Lebanon.
Wakati huo huo, vikosi vya jeshi la Israel vinaendelea na operesheni ya kukabiliana na wapiganaji wa Kundi la kigaidi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Netanyahu, achilia mbali tuhuma za rushwa na ukosolewaji kwa kuiingiza nchi kwenye vita, afya yake nayo imekuwa ikizua mijadala mingi katika miaka ya hivi karibuni.
Tangu aliporejea madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, Netanyahu amelazwa mara kadhaa hospitalini, kwa mujibu wa Ofisi yake.
Machi, 2024, alifanyiwa upasuaji wa hernia. Kabla ya hapo, Julai, 2023, Waziri Mkuu huyo alipandikiziwa kifaa maalumu baada ya kulalamikia hali ya usingizi wa mara kwa mara.
Baadaye mwaka huo, Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) ilitaka Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi, Yoav Gallant, wakamatwe kwa makosa ya uhalifu wa kivita huko Gaza.
Je, ni ipi nafasi yake ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27, 2026? Makala haya yanaeleza.
Katika utafiti uliofanyika hivi karibuni, upinzani umepewa nafasi kubwa ya kupata viti 61 vinavyohitajika kuunda Serikali.
Kupitia utafiti huo, asilimia 55 ya wananchi walisema wanatamani kuona Waziri Mkuu huyo akistaafu siasa, kwa mujibu wa Gazeti la Maariv la Israel.
Aidha, kati ya watu 502 waliohojiwa katika utafiti huo wa Taasisi ya Lazar, ni asilimia 38 pekee walioonesha kuwa na imani na kiongozi huyo.


