27.2 C
New York

Ronald Araujo: Beki wa kadi nyekundu aliyetua Liver akitokea La Liga

Published:

MERSEYSIDE, Uingereza

NYOTA huyo wa eneo la ulinzi ameondoka Barcelona na kujiunga na Liverpool majira haya ya kiangazi. Alikuwa nahodha wakati Wacatalunya hao wakitwaa ubingwa wa La Liga msimu uliopita (2025-26).

Kwa mujibu wa mkataba wake wa mkopo, Liverpool itaweza kumsajili moja kwa moja mwishoni mwa msimu wa 2026-27 endapo itavutiwa naye. Huyo ni Ronald Araujo.

Ifahamike kuwa kocha mpya wa Liverpool, Andoni Iraola, alihitaji beki wa kati anayeweza pia kucheza upande wa kulia, sifa ambazo Araujo anazo.

Kwa nafasi ya beki wa kulia, ujio wake ni faraja kwa mashabiki wa Liverpool, hasa kipindi hiki Conor Bradley, Joe Gomez na Giovanni Leoni wakiendelea kuuguza majeraha yao.

Vilevile, Araujo ataweza kutumika beki wa kati wakati huu Liverpool ikiwa imempoteza Ibrahima Konate aliyetimkia Real Madrid. Kwa ufupi, anakwenda kucheza ‘pacha’ na Virgil van Dijk.

Araujo alisajiliwa na Barcelona akitokea Boston River ya nchini kwao, Uruguay, mwaka 2018, na ameondoka akiwa amecheza mechi zaidi ya 200.

Msimu uliopita, alikuwa nahodha wa kikosi, akicheza mechi 38 chini ya kocha raia wa Ujerumani, Hansi Flick, ambaye amesema Araujo ni miongoni mwa wachezaji bora.

Kwa upande mwingine, zipo kumbukumbu mbaya za maisha yake ndani ya Barcelona. Miongoni mwazo ni kadi nyekundu aliyolimwa katika mchezo dhidi ya PSG (robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya) mwaka 2024.

Vilevile, kiwango alichokionesha katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa (dhidi ya Inter Milan) mwaka 2025 kilikosolewa na wengi, ingawa kocha Flick alimkingia kifua.

Pia, msimu uliopita alilimwa kadi nyekundu ya kipindi cha kwanza wakati Barcelona ikinyukwa mabao 3-0 na Chelsea katika mechi ya Ligi ya Mabingwa iliyochezwa katika Uwanja wa Stamford Bridge.

Wiki moja baada ya mechi hiyo, alipewa mapumziko ya kushughulikia changamoto ya afya ya akili. Alirudi uwanjani mwezi mmoja baadaye na kucheza mechi 23 za mwishoni mwa msimu, sita akianza katika kikosi cha kwanza.

Related articles

Recent articles