NEW YORK, Marekani
SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeeleza katika ripoti yake kuwa wasichana takribani milioni 2.4 nchini Afghanistan wamenyimwa haki ya kupata elimu ya sekondari.
Kwa mujibu wa UNESCO, kizingiti hicho kwa watoto wa kike ni tangu Kundi la Taliban liliporejea madarakani mwaka 2021.
Katika ripoti yake, Shirika hilo limedai kuwa idadi ya sasa ni ongezeko la wasichana 200,000, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2025.
Aidha, UNESCO imeonya kuwa huenda idadi ya watoto wa kike wanaozuiwa kuingia sekondari ikafikia milioni nne ifikapo mwaka 2030.
“Afghanistan ni nchi pekee duniani ambayo wanawake na watoto wa kike wanazuiwa kwenda sekondari na elimu ya juu,” amesema Mratibu wa Programu za Elimu na Dharura wa UNESCO, Hoda Jaberian.


