KINSHASA, DRC
WATAALAMU wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) wameonya kuwa wanawake ndilo kundi lililo hatarini zaidi kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini DRC.
Wakati huo huo, zipo taarifa kuwa visa viwili vya Ebola vimeripotiwa huko Amerika ya Kusini katika nchi ya Brazil.
Kwa DRC, maambukizi mengi kwa siku za hivi karibuni yameripotiwa kwa wanawake, hali inayoibua kuhitaji kwa tahadhari kubwa kwa kundi hilo.
Idadi ya jumla ni visa 282 nchini DRC, huku majimbo yaliyoathirika zaidi yakiwa ni Ituri, na Kivu ya Kaskazini na Kusini.
Kwa mujibu wa WHO, idadi ya wanawake waliofariki kwa Ebola nchini DRC ni kubwa kuliko miaka 50 iliyopita.
Kuhusika kwa wanawake katika vifo vingi kunatokana na kundi hilo kubeba mzigo mkubwa wa kuhudumia wagonjwa.
“Wauguzi (hospitalini) mara zote ni wanawake. Kama anahudumia, ni wazi yuko hatarini kupata virusi na kuvisambaza kwa alio karibu naye,” imeeleza taarifa ya WHO.
Majirani zao, Uganda, nao wako kwenye hatari, ikielezwa kuwa tayari visa vya maambukizi vimefikia tisa kwa sasa.


