20.9 C
New York

Serikali yatambua mchango wa JET katika uhifadhi wa mazingira

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

SERIKALI kupitia Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetunuku Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) tuzo maalum ya umahiri kwa kutambua mchango wake katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya mazingira nchini.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, akiwa na tuzo hiyo.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa Mei 28, 2026 kwa Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Chikomo amesema ni heshima kubwa kwa wanachama wote wa JET na uthibitisho kuwa kazi ya waandishi wa habari za mazingira inatambuliwa na serikali pamoja na wadau wa mazingira.

“Hii ni ishara kuwa mchango wa waandishi wa habari katika kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira unatambuliwa,” amesema Chikomo.

Ameeleza kuwa kwa miaka mingi JET imekuwa mstari wa mbele kuandika habari za mazingira kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Chikomo amesema tuzo hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi na weledi katika kuandika habari za mazingira huku akibainisha kuwa JET inaendelea kujipanga kuimarisha zaidi mchango wake katika sekta hiyo.

JET ilikabidhiwa tuzo hiyo na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, katika siku ya kwanza ya kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC.

Related articles

Recent articles