Na mwandishi wetu, Gazetini
MEI 23, kama ambavyo hufanyika kila mwaka, Dunia inaadhimisha Siku ya Fistula itokanayo na uzazi, ambayo husababisha kwa asilimia 90 visa vya watoto wanaozaliwa wakiwa wameshafariki.
Aidha, fistula ya uzazi huchangia asilimia 8% ya vifo vya uzazi, huku takwimu zikionesha kuwa wanawake na wasichana wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia na Pasifiki, nchi za Kiarabu, Amerika Kusini na Caribbea ndiyo wahanga wakubwa zaidi.
Licha ya kwamba haibagui umri, wasichana wadogo wako katika hatari zaidi kwa sababu miili yao inaweza kuwa haiko tayari kwa kujifungua. Je, fistula ya uzazi ni nini? Ni shimo linalotokea kati ya njia ya uzazi na kibofu ambayo husababisha kutoweza kudhibitiwa kwa mkojo.
Wakati mwingine, shimo hutokea kati ya njia ya uzazi na njia ya haja kubwa na kusababisha kinyesi kuvuja bila kujizuia.
Je, husababishwa na nini? Wataalamu wanaeleza kuwa chanzo cha fistula ya uzazi ni mama kuugua uchungu kwa muda mrefu kabla ya kujifungua.
Kwamba shinikizo la muda mrefu la kichwa cha mtoto kwenye njia ya uzazi hukata mfumo wa usambazaji wa damu na kusababisha mishipa kufa na kuanguka.
Lakini, aina zingine za fistula ya uzazi husababishwa na taratibu za upasuaji, aidha kwa uhaba wa vifaa au ujuzi mdogo wa zoezi hilo.
Nini madhara yake? Uwepo wa shimo hilo huweza kusababisha maambukizi, vidonda vyenye maumivi makali, magonjwa ya figo, ugumba na hata kifo.
Aidha, wanawake wenye tatizo hilo hupata changamoto za kutengwa na jamii kutokana na harufu mbaya itokanayo na uvujaji wa mara kwa mara wa mkojo au kinyesi.
Fistula ya uzazi inatibika? Ndiyo. Endapo tatizo litagundulika mapema, uwezekano wa kupona ni mkubwa kuliko kubaki na ugonjwa wa kudumu au kupoteza maisha.
Maseray Bangula raia wa Sierra Leone, ni miongoni mwa waliofanyiwa upasuaji wa fistula ya uzazi na kuondokana kabisa na tatizo hilo.
“Heshima yangu na utu wangu vimerejeshwa,” alisema Bangura, ambaye alifanyiwa upasuaji katika Kituo cha Wanawake cha Aberdeen mjini Freetown.


