Na Hassan Mwasha
ZIPO sababu nyingi za kukufanya uchukue hatua sasa ya kuachana kabisa na mkaa au kuni na kuhamia nishati safi ya kupikia katika matumizi yako ya kila siku hapo nyumbani.
Ukiachana na gharama kubwa, uchafuzi wa mazingira na ugumu wa upatikaji wake, matumizi ya mkaa au kuni yamekuwa yakisababisha changamoto za kiafya ya mtuamiaji kwa kuathiri mfumo wa upumuaji.
Habari njema zaidi, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Mafanikio hayo yametokana kwa kiasi kikubwa na hatua ya Serikali kuanzisha miradi ya utoaji wa ruzuku katika mitungi ya majiko katika kaya zilizoko vijijini.
Sambamba na hilo, pia imekuwapo miradi ya utoaji majiko ya umeme kupitia bili ya umeme (on-bill finance), jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watumiaji.
Akizungumza hivi karibuni katika Mdahalo wa Nishati Safi uliofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.), alisema:
“Ongezeko hilo limechangiwa na hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034,” alisema.
Wakati huo huo, Waziri Ndejembi alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wananchi.
Aidha, katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na nishati safi ya kupikia, Shirika la Umeme nchini (TANESCO) linajivunia mafanikio makubwa ya mfuko wa mikopo ya majiko kwa wateja wake.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, akisema utaratibu huo ulifakiwa kwa asilimia 95.
“… Sisi tumetengeneza ubia na wasambazaji binafsi, ambapo tunakwenda sasa kukopesha majiko milioni moja,” alisema Bw. Twange.
“Mpango huo ni sehemu ya juhudi za TANESCO kuongeza matumizi ya umeme kama nishati safi ya kupikia na kuwawezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa utaratibu unaorahisisha uwezo wao wa kumudu gharama.”
Katika hatua nyingine, aligusia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya TANESCO na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa umeme Visiwani humo.
Mpango huo ni utekelezaji wa mradi wa kuongeza kiwango cha umeme kinachosafirishwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme katika visiwa hivyo.
“Tuna mradi wa kuongeza kiwango cha umeme unaotoka Tanzania Bara kuja huku. Tumepata mdau wa maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dola za Marekani milioni 282 (zaidi ya Sh bil. 600 za Tanzania).
“Tunakwenda kutengeneza njia tatu za kupita chini ya maji, moja kuja Unguja, nyingine kwenda Pemba na nyingine kwenda Mafia,” alisisitiza Bw. Twange.


