Na Mwandishi Wetu, Gazetini
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekusanya Sh.trilioni 26.63 katika kipindi cha July 2025 hadi February, 2026 kati ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 25.68, sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 na ukuaji wa asilimia 19.27 ikilinganishwa na mapato ya Sh. trilioni 22.32 yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.
Mwigulu amesema hayo leo April Mosi 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2026/2027.
Amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza makusanyo ambapo mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kupanua wigo wa kodi na kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato.
“Kati ya mapato hayo, shilingi trilioni 22.09 ni mapato yaliyotokana na kodi, shilingi trilioni 3.78 ni mapato yasiyo ya kodi na shilingi bilioni 754.26 ni misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo, kati ya fedha zilizokusanywa, shilingi trilioni 12.28 zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa SGR, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya na elimu, miradi ya maji, miundombinu ya Nishati, Usafiri na usafirishaji; na Skimu za umwagiliaji,” amesema.
Wakati huo huo Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya Sh. trilioni 12.5 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Dk. Mwigulu amesema kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 8.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. trilioni 3.7 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.


