LONDON, Uingereza
ALIYEWAHI kuwa mmiliki wa klabu ya Nottingham Forest ya Ligi Kuu ya England (EPL), Fawaz Al-Hasawi, anaendelea vizuri baada ya kuvamia na kujeruhiwa na majambazi.
Taarifa zinaeleza kuwa watu walioficha nyuso zao kwa ‘mask’ waliingia mjengoni kwake na kumkuta bilionea huyo akiwa amelala.
Majambazi hao walivamia mjengo wake wa mjini Mayfair, ambao vyanzo mbalimbali vya habari vinautaja kuwa na thamani ya Pauni milioni 10.
Katika purukushani, Al-Hasawi mwenye umri wa miaka 57 alichomwa na kitu chenye ncha kali mkononi na shingoni.
Bosi huyo raia wa Kuwait, alikuwa mmiliki wa Nottingham Forest kuanzia mwaka 2012 hadi 2017. Aliiuza kwa tajiri wa sasa, Evangelos Marinakis.
Ikiwa Daraja la Kwanza (Championship) wakati huo, timu hiyo ilipita chini ya makocha watano, kabla ya mmiliki mpya, Marinakis, kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2022.


