Na mwandishi wetu, Gazetini
VITENDO vya ugaidi vimeendelea kuwa tishio kwa usalama wa dunia, kwa mujibu wa Taasisi ya kimataifa ya Uchumi na Amani (IEP).
Kwa mujibu wa ripoti yake ya mwaka huu iliyochapishwa katika mtandao wa World Visualized, matukio ya ugaidi yameshuhudiwa katika mataifa 66 duniani kwa mwaka 2024 pekee.

Takwimu hizo zinathibitisha ongezeko la matukio ya ugaidi, ukilinganisha na mwaka 2023, ambapo ni nchi 58 zilizokuwa zimeripotiwa kuwa na changamoto hiyo.
Kwamba kwa sasa ni nchi nane zimeongezeka ndani ya kipindi cha mwaka mmoja pekee (2023-24). Ni ongezeko kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2017.
Takwimu zinazitaja nchi za Ukanda wa Sahel kuwa ndizo zilizoathirika zaidi na matukio ya kigaidi. Mataifa hayo ni pamoja na Burkina Faso, Mali na Niger.
Lawama nyingi zinaelekezwa kwa vikundi vilivyo chini ya magaidi wa ISIS, ambavyo vimeendeleza mashambulizi Mashariki ya Kati na baadhi ya maeneo ya Afrika.


