Na mwandishi wetu, Gazetini
HUKU ikionekana kuwa ni kwenda na wakati, utamaduni wa watoto kuachiwa ‘simu-janja’ (smartphone) una madhara mkubwa kwao, utafiti wa hivi karibuni unaeleza.
Kikichowasukuma wataalamu wa afya kufanya utafiti huo ni kutaka kujua uhusiano uliopo kati ya afya za watoto na mtumizi yao ya ‘smartphone’.
Kufanikisha utafiti uliochapishwa katika Jarida la Afya la Pediatrics, wataalamu hao walihusisha watoto zaidi ya 10,600 waliokuwa wanamiliki simu hizo za kisasa.
Ni katika utafiti huo, asilimia 64 ya watoto wenye umri wa miaka 12 walikiri kuwa ni wamikiki halali kwa kununuliwa simu hizo na wazazi wao. Asilimia 84 ya wamiliki wa simu walikuwa ni watoto wenye umri wa miaka 14.
Aidha, utafiti ulibaini kuwa watoto wote hao wanatumia wastani wa zaidi ya saa tano kwa siku wakiwa ‘bize’ kwenye vioo vya simu zao.
Kwa utafiti huo, ndipo walipobaini kuwa watoto wenye umri wa miaka 14 au chini ya hapo, wako hatarini zaidi endapo watazoea kutumia simu hizo za kisasa.
Utafiti huo umeenda mbali zaidi na kueleza kuwa watoto wa aina hiyo hujikuta kwenye changamoto za msongo wa mawazo, kuongezeka uzito na kukosa usingizi hapo baadaye.
Kati ya hao, asilimia 30 walionekana kupitia nyakati za changamoto ya msongo wa mawazo kupitia simu zao.
Wataalamu wamegundua kuwa simu huwafanya watoto kujitenga na kukosa muda wa kujumuhika na wenzao, hivyo kukaribisha msongo wa mawazo.
Wakati huo huo, kutokana na ‘ubize’ wa simu, asilimia 60 walionekana kushindwa kupata muda wa kutosha wa kulala.
Vilevile, asilimia 40 walioonekana kuwa hatarini kupata ongezeko la uzito ni kutokana na kutumia muda mwingi kwenye simu, hivyo mwili kubweteka.
Hata hivyo, watafiti hawakatazi moja kwa moja matumizi ya simu-janja kwa watoto, bali wanawataka wazazi kuwa nao karibu ili kuepuka matumizi ya kiwango kikubwa yanayoweza kuathiri afya zao.


