10.9 C
New York

UNICEF: Vikwazo vya umri pekee havitoshi kuwalinda watoto mitandaoni

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

ULIMWENGUNI kote, serikali zinaendelea kujadili umri unaofaa kuruhusu matumizi ya mitandao ya kijamii, huku baadhi zikianzisha vikwazo vipya vya umri ili kuongeza usalama wa watoto mtandaoni.

Hatua hizi zimechochewa na ongezeko la vitisho ikiwemo ukatili wa mtandaoni, unyanyasaji, unyonyaji na maudhui hatarishi yanayoathiri afya ya akili na ustawi wa watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) limeeleza kuwa mfumo wa sasa haujalinda kikamilifu haki na usalama wa watoto, na badala yake umeacha mzigo mkubwa kwa wazazi ambao mara nyingi hawana zana za kutosha kuwasaidia watoto katika mazingira ya kidijitali.

Vikwazo vya umri ‘si suluhisho kamili’

UNICEF imesema licha ya kuunga mkono jitihada za serikali kulinda watoto, kutegemea marufuku za umri pekee kunaweza kuleta madhara. Kwa watoto wengi, mitandao ya kijamii ni njia muhimu ya kupata elimu, kujieleza, kuunganishwa na wenzao na kujenga uthubutu, hasa kwa walio katika mazingira magumu.

Shirika hilo limeonya kwamba hata kwa kuweka vizuizi, watoto bado wanaweza kutumia njia mbadala au majukwaa yasiyodhibitiwa, hivyo kuongeza hatari. Limeeleza kuwa sheria za umri zinapaswa kuunganishwa na sera pana zinazolinda haki za watoto, faragha na ushiriki wao salama mtandaoni.

UNICEF pia imesisitiza kwamba vikwazo pekee haviwezi kuchukua nafasi ya wajibu wa makampuni ya teknolojia kuboresha miundo ya majukwaa, kuhakikisha udhibiti bora wa maudhui na kutengeneza mifumo rafiki kwa watoto.

Wito kwa Serikali

Katika mapendekezo yake, UNICEF imetoa wito kwa serikali, wadhibiti wa masuala ya kidijitali na makampuni teknolojia kushirikiana na watoto pamoja na familia zao ili kujenga mazingira salama na jumuishi mtandaoni.

Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni, kutaka makampuni yaweke uwekezaji wa lazima katika usalama wa majukwaa, ikiwemo udhibiti wa maudhui, kubuni majukwaa yanayozingatia usalama wa watoto na kutumia mifumo ya kuthibitisha umri inayolinda haki zao.

Nyingine ni wadhibiti kuweka hatua madhubuti za kuzuia madhara ya mtandaoni, jamii na wadau kusikiliza kwa makini sauti na uzoefu wa watoto, vijana, wazazi na walezi katika utoaji maamuzi kuhusu kanuni za umri.

Kutoa msaada na elimu kwa wazazi ili kuongeza uelewa wa kidijitali, kwani wao mara nyingi hubeba jukumu gumu la kuwalinda watoto katika mifumo ambayo hawakuiunda.

UNICEF imesema itaendelea kushirikiana na serikali, sekta binafsi na jamii kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza, kuunganishwa na kustawi kwa usalama katika zama hizi za kidijitali zinazobadilika kwa kasi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img