WASHINGTON DC, Marekani
NI agizo la Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema hataki kuona wahamiaji wa Somalia wakiingia na kuishi nchini kwake. Katika Mkutano wake na Baraza la Mawaziri, Rais Trump alienda mbali zaidi na kusema Marekani haiwezi kuwa kimbilio la ‘takataka’.
Wakati huo huo, alisema wahamiaji wa Somalia walioko Marekani wanapaswa kufungasha virago na kurejea walikotoka. “Siwataki katika nchi yetu. Lazima niseme ukweli. Litakuwa ni kosa ikiwa tutaendelea kuwa na takataka kwenye nchi yetu,” alisisitiza.
Kauli ya Rais Trump inakuja wakati huu mamlaka za uhamiaji nchini Marekani zikiwa zimeshatangaza operesheni katika maeneo wanayoishi Wasomali wengi mjini Minnesota.
Ifahamike kuwa Minnesota, kama ilivyo kwa St Paul, ndiyo miji inayoongoza kwa idadi kubwa ya Wasomali wanaoishi Marekani.
Baada ya viongozi wengi wa Serikali ya Marekani kuikosoa hatua hiyo ya Trump, Rais huyo amewajibu akisema:
“… Najua wapo watakaosema haijakaa sawa kisiasa, lakini wala sijali. Ninachosema ni kwamba siwahitaji (Wasomali) katika nchi yetu.”


