5.7 C
New York

Mgonjwa adaiwa kubakwa na tabibu, watatu wasimamishwa kazi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WATUMISHI watatu wa kada ya afya, akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo, wamesimamishwa kazi kufuatia sakata la mgonjwa kudaiwa kubakwa na tabibu wa hospitali ya wilaya hiyo, huku wengine wawili wakiendelea kuhojiwa kwa tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa maadili ya kazi.

Hatua hiyo imetangazwa leo Desemba 1, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, wakati wa ziara maalum ya Kamati ya Usalama ya Mkoa katika Wilaya ya Urambo. Ziara hiyo ilifanyika kufuatia matukio kadhaa ya utoaji huduma duni katika baadhi ya vituo vya afya, ikiwemo tukio la ukatili lililoripotiwa kutokea Novemba 24, 2025.

Tukio hilo lililowashitua wengi lilikuja wazi baada ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuagiza kusimamishwa kazi kwa tabibu anayetuhumiwa, akisisitiza kuwa uchunguzi wa kina ufanyike ili kuchukua hatua stahiki.

“Haiwezekani wananchi wapate huduma zisizoeleweka. Mtuhumiwa inaonekana tayari alikuwa na rekodi ya tabia zisizofaa hata katika kituo alichotoka,” alisema RC Chacha.

Maelezo ya Mgonjwa

Mwanamke aliyetajwa kudhalilishwa (jina lake limehifadhiwa kwa sababu za faragha) alisema alifika hospitalini na mume wake kutafuta huduma ya afya ya uzazi. Alidai kuwa tabibu aliyemhudumia alimpeleka katika chumba cha upasuaji kwa ajili ya matibabu ya kina, ambapo tukio la unyanyasaji lilitokea.

Alisema alishtuka baada ya taratibu ya matibabu aliyoelekezwa kutofuatwa ipasavyo, jambo lililosababisha kutoa taarifa hiyo kwa familia yake na baadaye kwa uongozi wa hospitali.

Kauli ya Familia

Mama mzazi wa mwanamke huyo alisema alipokea taarifa kutoka kwa binti yake akiwa nyumbani, na mara moja alifika hospitalini kutoa taarifa za tukio hilo.

“Nimeumia sana. Mwanangu alienda kupata huduma, lakini akakutana na jambo la kumvunja moyo. Mpaka sasa hajaendelea kupata matibabu anayohitaji kutokana na tatizo lake,” alisema. Uchunguzi wa kina unaendelea, na uongozi wa mkoa umeahidi kuhakikisha hatua za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img