14 C
New York

Simba v Atletico; Pantev ana kwa ana na kocha Barcelona

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

NI Simba ya kocha Dimitar Pantev dhidi ya Petro Atletico katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi unaotarajiwa kuchezwa Novemba 21, mwaka huu. Wekundu wa Msimbazi wataanzia nyumbani.
Ikumbukwe, Simba wako Kundi D msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, ambapo wamepangwa na Petro, ES Tunis (Tunisia) na Stade Malien.

Baada ya kufika robo fainali misimu miwili mfululizo ya hivi karibuni, safari hii Wekundu wa Msimbazi watahitaji kupiga hatua moja (nusu fainali) au mbili zaidi (fainali). Je, ni nani hao Petro Atletico? Makala haya yanawachambua mabingwa hao mara 19 wa taji la Ligi Kuu ya Angola. Karibu.

Mosi, Petro ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Angola kwa misimu yote minne ya hivi karibuni (2021-2022, 2022-23, 2023-24 na 2024-25). Pili, hii ni mara yao ya nane kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na mafanikio makubwa zaidi kwao ni kufika nusu fainali mara mbili, ikiwamo msimu wa 2021-22.

Tatu, kabla ya kuifuata Simba, Petro Atletico watacheza mechi yao ya Ligi dhidi ya Kabuscorp, inayotarajiwa kuchezwa Novemba 18, mwaka huu. Nne, msimu huu, Petro Atletico inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Angola, nyuma ya Kabuscorp, Primeiro de Agosto, Wiliete ma CRD Libolo inayoongoza.

Tano, katika mechi sita ilizocheza msimu huu wa Ligi, imeshinda nne na kufungwa mbili, ikikusanya pointi 12.
Sita, katika mechi sita, imefunga mabao 10 lakini safu yake ya ulinzi imeruhusu nyavu kutikiswa mara saba.
Saba, wakati Simba ikiwa imetoka kuirarua JKT kwa mabao 2-1, Petro Atletico walifungwa bao 1-0 na Primeiro de Agosto katika mchezo uliopita.

Nane, Petro Atletico wamefika hatua ya makundi msimu huu kwa kuitoa Stade d’Abidjan (4-0) na Cercle De Joachim (6-0). Tisa, kocha wao ni raia wa Hispania, Franc Artiga, ambaye aliwahi kufanya kazi kwa miaka 10 ndani ya kituo cha vipaji vya soka cha Barcelona, La Masia. Mwisho, Petro Atletico ni waumini wa soka la kasi na pasi nyingi, wakitumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img