6.4 C
New York

Utafiti: Sokwe nao ni walevi wa pombe kama binadamu

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
KAMA ulidhani binadamu ndiye kiumbe pekee kinachotumia kilevi aina ya pombe hapa duniani kwa ajili ya starehe au kupoteza mawazo, basi hakuna unachokijua. Sokwe nao wamo!
Utafiti wa Chuo Kikuu cha California nchini Marekani umebaini hivyo, kwamba wanyama aina ya sokwe, ambao kimsingi ni jamii ya mamalia kama binadamu, nao ni watumiaji wazuri tu wa pombe.
Tofauti na binadamu wanaokwenda kununua, utafiti huo ulioongozwa na Aleksey Maro umebaini kuwa sokwe hupata pombe kupitia aina fulani ya matunda yaliyopo porini.
Watafiti waliifanyia utafiti aina 20 ya matunda katika hifadhi kubwa mbili barani Afrika, ambazo ni Kibale ya Uganda na Tai ya Ivory Coast.
Katika utafiti wao, ndipo walipogundua kuwa matunda hayo yana kilevi cha hadi asilimia 0.3. “Kwa siku, sokwe hutumia matunda hayo kwa wastani wa chupa moja ya bia,” inaeleza ripoti ya utafiti.
“Ndiyo, sokwe hutumia takribani kilo 4.5 ya matunda hayo kila siku. Ukilinganisha na uzito wa sokwe, ambao ni takribani kilo 41, ni sawa na binadamu anayekunywa nusu lita ya bia.”
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa wanyama aina ya sokwe kuhusishwa na matumizi ya pombe. Upo utafiti wa Chuo Kikuu cha Exeter uliofanyika katika Hifadhi ya Cantanhez nchini Guinea-Bissau.
Kupitia kamera, watafiti walinasa matukio 70 ya sokwe wakila kwa pamoja matunda yenye kilevi hicho. Mkusanyiko huo ulihusisha sokwe wa umri na jinsia zote.
Wakati huo, watafiti wa Chuo Kikuu cha Exeter walibaini kuwa matunda hayo ya Hifadhi ya Cantanhez yalikuwa na kilevi cha hadi asilimia 0.61.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img