Na Samwel Mwanga, Maswa
Katika kijiji cha Dulungwa, wilayani Maswa mkoani Simiyu, wanawake wengi wanaishi kwa wasiwasi na mkanganyiko kuhusu matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Licha ya serikali kusambaza dawa na vifaa vya kutosha katika zahanati na vituo vya afya, idadi ya wanaotumia huduma hizo bado ni ndogo ikisababisha kuongezeka kwa ujauzito usiopangwa.
Kwa mujibu wa taarifa za Idara ya Afya wilayani Maswa, kati ya wanawake 10 wanaojifungua kila mwezi,wanne hadi watano wanaripoti kuwa hawakupanga kupata ujauzito. Idadi hiyo inahusishwa moja kwa moja na kushuka kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hasa vijijini.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Makala hii, umebaini kuwa hofu na mitazamo ya kidini ni miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya wanawake wengi, hasa wa vijijini, kuacha au kutoanza kabisa kutumia njia hizo.
Agness Mboje ni mama wa watoto sita mkazi wa kijiji cha Dulungwa, anasema aliwahi kupewa elimu ya uzazi wa mpango katika zahanati ya kijiji, lakini alishindwa kutumia kwa kuamini kuwa ni kumpinga Mungu.

“Niliambiwa na kiongozi wetu wa dini kuwa kutumia dawa za kupanga uzazi ni sawa na kuzuia mpango wa Mungu. Nilihofia nikienda kinyume nitapata laana, hivyo nikaacha,” anasema.
Kwa sasa Agnes analalamika kuwa watoto wake wanateseka kwa kukosa mahitaji ya msingi, lakini bado anasita kutumia njia yoyote akisema, labda Mungu mwenyewe atanisaidia.
Naye Aisha Zengo mkazi wa kijiji hicho anasema alikuwa akitumia sindano ya depo lakini aliacha baada ya kusikia mafundisho ya dini katika makambi ya kanisa analoabudu, kwamba sindano hiyo husababisha wanawake kukosa hedhi kwa muda mrefu na kuathiri uwezo wa kupata mtoto baadaye.
“Nilihofia kuendelea kutumia. Nilihisi kama mwili wangu umebadilika, nikaamua kuacha kabisa. Miezi michache baadaye nikabeba ujauzito bila kutarajia,”anasema Aisha.
Kauli ya viongozi wa dini
Mchungaji mstaafu,Traifan Nkya ambaye ni msaidizi wa Askofuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, anasema baadhi ya viongozi wa dini bado hawajapata uelewa mpana wa uzazi wa mpango, jambo linalowafanya kuwahubiria waumini kwa mtazamo wa kiimani zaidi kuliko wa kiafya.
“Sisi kama viongozi wa dini tunatakiwa kuelewa kwamba kupanga uzazi si kupinga mapenzi ya Mungu, bali ni kujali afya ya mama na ustawi wa familia. Tatizo ni kuwa baadhi ya viongozi hawana taarifa sahihi,” anasema Mchungaji Nkya.
Kwa upande mwingine, Sheikh Issa Eliesa wa Baraza Kuu la WaislamuTanzania (BAKWATA), wilayani Maswa, anasema Uislamu haukatazi kupanga uzazi, mradi unafanyika kwa makubaliano ya wanandoa na si kwa nia ya kuua kizazi.
“Tunachokataza ni utoaji mimba au kutumia njia zenye madhara. Lakini kupanga uzazi kwa njia salama, ili kuimarisha afya ya mama na malezi ya watoto, Uislamu unaruhusu,” anasema Sheikh Issa.
Watumishi wa afya vijijini walia
Katika zahanati ya kijiji cha Dulungwa, Muuguzi Christina Maduhu anasema idadi ya wanawake wanaoomba huduma ya uzazi wa mpango ni ndogo, na wengi wao hujitokeza kwa usiri mkubwa.
“Wengine waomba huduma kwa siri kabisa. Wanaogopa waume zao, wazazi au viongozi wa dini wasijue na baadhi hukimbia wakiona mtu anayewafahamu akiingia kliniki,” anasema Christina.
Anasema tatizo lingine ni upotoshaji unaotokana na mitandao ya kijamii na vikao vya kijamii, ambapo wanawake huambiwa njia hizo zinaua damu au zinatengeneza uvimbe tumboni jambo ambalo si kweli.
Uelewa bado ni changamoto
Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto wilayani Maswa,Sakina Mkwende, anasema licha ya serikali kusambaza vifaa vya uzazi wa mpango vya kutosha kutoka Bohari ya Dawa (MSD), kiwango cha matumizi hakijafika hata nusu ya malengo ya kitaifa.
“Tunapata depo, tembe, na vipandikizi kwa wingi, lakini wanawake wachache wanajitokeza. Hofu na imani potofu zimekuwa kikwazo kikubwa kuliko upatikanaji wa dawa,” anasema.
Ngaiza anasema wilaya sasa inatekeleza mpango maalum wa kutoa elimu ya uzazi wa mpango kupitia vikundi vya akinamama na viongozi wa dini, ili kuondoa hofu na mitazamo hasi.
Ushuhuda wa wanawake waliofanikiwa
Neema Masumbuko, mkazi wa kijiji cha Malita, anasema alianza kutumia kipandikizi baada ya kupata elimu ya kina kutoka kwa muuguzi.
“Nilikuwa na hofu mwanzoni, lakini nilipewa elimu sahihi. Sasa nina watoto wawili, ninaweza kupanga maisha vizuri na afya yangu ni nzuri,” anasema Neema.
Wito wa wataalam
Daktari wa afya ya uzazi Dk.Deogratius Mtaki ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa anasisitiza kuwa suluhisho la kudumu ni kuunganisha elimu ya afya na imani.
“Tukishirikisha viongozi wa dini, wazee wa kimila, na watumishi wa afya kwa pamoja, tutaweza kuondoa hofu. Watu waelewe kuwa kupanga uzazi ni sehemu ya kumheshimu Mungu kwa kulinda uhai,” anasema.
Dk Mtaki anasema njia za kisasa za uzazi wa mpango ni salama na zimepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa sindano, tembe au vipandikizi vinamsababishia mwanamke utasa. Hofu hizi ni matokeo ya kukosa elimu sahihi,” anasema.
Anasisitiza kuwa kila mwanamke anatakiwa kuchagua njia inayomfaa baada ya ushauri wa kitaalamu, badala ya kuiga wengine au kuamua kwa kusikia maneno ya mitaani.
Hofu, imani potofu na upotoshaji kuhusu njia za uzazi wa mpango zimeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wa wilaya ya Maswa, wengi wao wakijikuta wakibeba ujauzito usiopangwa.
Wataalam wanatoa rai ya kuimarisha elimu endelevu inayowahusisha viongozi wa dini, jamii na familia si hospitali pekee ili kubadilisha mitazamo hiyo na kuokoa afya za wanawake na familia.


