MADRID, Hispania
BAADA ya miezi mingi ya tetesi, ni rasmi sasa Yan Diomande amejiunga na Real Madrid akitokea RB Leipzig ya Ligi Kuu nchini Ujerumani (Bundesliga).
Kiungo wa pembeni huyo alimaliza msimu uliopita (2025-26) akiwa amezifumania nyavu mara 12 katika mechi 33 za Ligi Kuu hiyo.
Diomande (19), ametua Madrid kwa dau la Pauni milioni 100, hivyo kuwa mchezaji wa bei mbaya zaidi kuwahi kuuzwa na RB Leipzig.
Wakati huo huo, winga huyo anakuwa mchezaji aliyenunuliwa kwa dau nono zaidi katika historia ya Madrid.
Kama hiyo haitoshi, raia huyo wa Ivory Coast anayecheza winga zote mbili anakuwa mchezaji ghali zaidi barani Afrika.
HAIKUWA RAHISI
Alizaliwa mjini Abidjan, Ivory Coast, na akiwa na umri wa miaka tisa alikuwa kwenye ‘academy’ ya Inter Foot Sud Comoe iliyoko mpakani mwa Ghana, umbali wa maili 70 kutoka nyumbani kwao.
Akiwa na miaka 15 tu, Diomande aliondoka Ivory Coast na kwenda Marekani kwa ajili ya kutafuta njia ya kutimiza ndoto zake za soka.
Hata hivyo, akiwa huko, hakuna klabu iliyokuwa ikifuatiwa naye. “Hata timu B za Marekani hazikunitaka. Sikujua sababu. Hawakuwa wakinipa sababu. Kila nilikokwenda niliambiwa hapana,” anasimulia Diomande.
Miongoni mwa klabu alizowahi kupita kwa ajili ya majaribio na kukosa nafasi ni Chelsea, Bournemouth, Crystal Palace, Rangers na Olympiacos.
Kibali cha kuishi (viza) Marekani kilipokwisha, Diomande alitakiwa kurudi Ivory Coast lakini ghafla alibahatika kusajiliwa na Leganes ya Hispania.
Akiwa na miaka 18, akacheza mechi yake ya kwanza ya La Liga kwa kuwavaa mabosi wake wa sasa, Madrid, katika Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Hata hivyo, dakika 90 za mchezo huo zilizomalizika, Diomande akapata pigo zito. Akapokea meseji ya kifo cha mdogo wake wa kike, Roxanne, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 15.
Chanzo cha kifo cha Roxanne hakikuelezwa, ingawa zipo taarifa zisizothibitika zikidai kuwa aliwekewa kitu kwenye kinywaji chake alipokuwa kwenye sherehe.
Mbali na taarifa mbaya hiyo, mechi dhidi ya Madrid ikafungua milango kwa Diomande na hatimaye Leipzig ikafikia mezani na kumsajili kwa euro milioni 20.
SHABIKI WA PSG, KAZI NA JAY Z
PSG ndiyo klabu aliyoishabikia tangu akiwa mdogo. Ni kwa sababu baba yake pia alikuwa shabiki wa matajiri hao wa soka la Ufaransa.
Kwa upande mwingine, Diomande anasimamiwa na kampuni ya uwakala ya Roc Nation inayomilikiwa na lejendari wa muziki wa Hip hop, Jay Z.
Inafahamika kuwa Roc Nation ndiyo kampuni inayowasimia pia mastaa wawili wa Madrid na timu ya Taifa ya Brazil, Vinicius Jr na Endrick.
Diomande alihamia Roc Nation baada ya kuachana na kampuni ya Maxidel inayomilikiwa na winga wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast, Max Gradel.


