PRETORIA, Afrika Kusini
AFRIKA Kusini inaweza kuwa Taifa la kwanza barani Afrika kupitisha sheria inayopiga marufuku biashara ya ukahaba, ingawa ugumu wa maisha, hasa kwa akina dada, unaweza kuwa kikwazo kikubwa.
Connie Mathe, ambaye alianza ‘kuuza’ ngono akiwa na umri wa miaka 19, anasema alijikuta kwenye biashara hiyo baada ya kushindwa kumudu gharama za maisha.
“Awali, ilianza kama urafiki na mwanaume mmoja, ambaye hata hivyo tayari alikuwa na familia yake, ameoa.
“Akawa ananitumia kila alipohitaji na kunipa fedha. Sikuelewa, ni hadi pale rafiki yangu aliponiambia kuwa ni kama nauza ngono kwa mwanaume huyo,” anasema Connie.
Bibiye huyo anasema alilazimika kujiingiza moja kwa moja katika biashara ya ‘kuuza mwili’ baada ya mwanaume huyo kusitisha huduma ya chakula na kodi. “Sikuweza tena kumudu maisha,” anasisitiza.
Kwa upande mwingine, Taasisi ya kutetea haki za makahaba ya SWEAT ya nchini Afrika Kusini nayo haikubaliani kwa namna yoyote ile na jitihada zinazoendelea za kukomesha biashara hiyo.
Septemba, mwaka huu, wanaharakati wa SWEAT walikusanyika nje ya Mahakama ya Cape Town wakiwa na mabango yenye jumbe za kupinga mchakato wa Kikatiba wa kupiga marufuku biashara ya ukahaba.
Kwa mujibu wa SWEAT katika mahojiano yake na DW, biashara ya ngono ni ajira kwa watu zaidi ya 150,000 nchini Afrika Kusini, huku asilimia 90 wakiwa ni wanawake.
SWEAT wanamtaja Connie kuwa ni mfano mdogo na halisi wa wanawake wanaoendesha maisha yao kupitia biashara ya ngono baada ya kupitia changamoto ya kushindwa kumudu gharama za bidhaa, kodi na mahitaji mengine.
Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2021, asilimia 70 ya makahaba nchini Afrika Kusini hawapo salama, na badala yake hukumbana na changamoto ya kunyanyaswa kijinsia wanapokuwa ‘kazini’.
Akihojiwa na DW, Connie anakiri kuwahi kudhalilishwa, ikiwamo kulazimishwa kukaa utupu ya polisi waliokuwa wamemkamata akiwa kwenye ‘mawindo’ yake nyakati za usiku.
Aidha, watafiti walibaini kuwa asilimia 60 wamekumbana na matukio ya kubakwa. “Mmoja kati ya saba walifanyiwa ukatili huo na polisi na wahanga huogopa kuripoti,” ilieleza taarifa ya utafiti huo.
Wakati huo huo, jitihada za kukomesha biashara ya ngono zimelenga kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Afrika Kusini inatajwa kuwa kinara wa ugonjwa huo duniani.
Kwa sasa, biashara ya ngono imeonekana kushika kasi duniani kote, ikiwamo Marekani. Hata hivyo, Ubelgiji na New Zealand ni mataifa pekee yaliyopiga marufuku biashara hiyo.
Ni tofauti na Ujerumani, Uholanzi, Peru na Senegal, ambako inaruhusiwa na zipo sheria za kuwalinda makahaba. Katika mataifa hayo, ukahaba ni ajira rasmi kama ilivyo ualimu, udaktari na nyinginezo.
Lakini, jumuhiya za kimataifa, zikiwamo Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), ,Amnesty International na Human Rights Watch, zinaunga mkono hatua ya kupiga marufuku biashara ya ngono duniani kote.
Published:


