Na mwandishi wetu, Gazetini
HUKUMU ya kifo aliyopewa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, imegonga vichwa vya habari za siasa barani Afrika kwa wiki za hivi karibuni.
Licha ya kwamba Kabila hakuwepo na wala hakuwa na uwakilishi, haikuizuia Mahakama ya Kijeshi kusoma hukumu hiyo iliyotokana na makosa mbalimbali, yakiwamo ya uhaini na uhalifi wa kivita.
Hukumu hiyo imeenda sambamba na faini ya Dola za Marekani bilioni 29 kwa Serikali, pia akitakiwa kulipa fidia ya jumla ya Dola bilioni 4 kwa athari za kivita alizosababisha katika maeneo mawili ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu.
Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa mahakamani, mwanasiasa huyo ni mshirika wa Kundi la waasi la M23, ambalo limeondosha kabisa hali ya usalama katika maeneo hayo ya Mashariki mwa DRC.
Ikumbukwe, tangu M23 lilianza vurugu zake na kukita mizizi katika Mji wa Goma mwanzoni mwa mwaka huu, watu 3,000 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine takribani milioni moja wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
Katika hilo, Kabila anatajwa kushirikiana kwa karibu na uongozi wa M23, ambao pia wanaelezwa kusaidiwa na Rwanda, huku mkakati wao ukiwa ni kumng’oa madarakani Rais Felix Tshisekedi.
Hata hivyo, hatua ya Serikali kumuhukumu kifo huenda ikahatarisha zaidi hali ya usalama nchini DRC, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa.
Si tu hukumu hiyo inaweza kutibua mazungumzo ya amani kati ya Serikali na waasi wa M23, bali pia imekwenda kuwagawa wananchi kutokana na ushawishi mkubwa alionao Kabila.
Kabila, ambaye alikuwa madarakani kuiongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, anafahamika kuwa ni mpinzani mkubwa wa kisiasa wa Rais Tshisekedi.
Hivyo, kwa wafuasi wake, huenda wakawa na mtazamo tofauti juu ya hukumu hiyo na kuamini kuwa ni matokeo ya ‘chuki’ za Rais Tshisekedi kwa mwanasiasa huyo.
Kwa upande wake, Kabila amekuwa akiibuka mara kadhaa na kudai kuwa mwenzake huyo anaitumia mahakama kuwaadhibu wale wanaokosoa uongozi wake.
Kabila (53), aliingia madarakani kuiongoza DRC akiwa na umri wa miaka 29 baada ya baba yake, Laurent Kabila, kuuawa akiwa rais wa nchi hiyo.
Uongozi wake ulioandamwa na kashfa nyingi za rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ulikomea mwaka 2016 lakini alivunja Katiba kwa kusogeza mbele Uchaguzi Mkuu, ambao hata hivyo ulifanyika mwaka 2018.
Ugomvi wake na Tshisekedi
Baada ya kupoteza kiti cha urais mbele ya Rais Tshisekedi mwaka 2018, Kabila alikubali matokeo lakini kwa makubaliano ya baadhi ya washirika wake kuwa sehemu ya Serikali mpya.
Kwamba baadhi ya wanasiasa wa Chama chake cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) wangepata nafasi za uongozi katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Rais Tshisekedi wa Union for Democracy and Social Progress (UDPS).
Lakini, ilipofika mwaka 2020, Rais Tshisekedi alisitisha ushirikiano huo kwa kuwaondosha katika Serikali yake washirika wa Kabila.
Mwishoni mwa mwaka 2021, Serikali ya DRC ilianzisha rasmi uchunguzi dhidi ya Kabila kwa madai ya utawala wake kujihusisha na vitendo vya rushwa. Hatua hiyo ilikuja baada ya mabadiliko ya Katiba yaliyoondosha kinga ya rais mstaafu kushitakiwa.
Ni kutokana na presha hiyo, Kabila alilazimika kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini, ingawa hajulikani aliko kwa sasa kutokana na hofu ya kutiwa nguvuni.
Lakini, kupitia Gazeti la Sunday Times, aliandika akisema Rais Tshisekedi hana mpango wa kuachia madaraka na ameshindwa kushughulikia mgogoro unaoendelea kati ya Serikali na M23.
Akijibu shutuma hizo, Rais Tshisekedi akiwa mjini Munich, alimtaja Kabila kuwa amekuwa akichangia fedha kulisaidia Kundi hilo la waasi.
Ni kweli anashirikiana na M23?
Kwa upande mwingine, hisia za Kabila kuwa sehemu ya M23 zinatokana na taarifa za ukaribu wake na kiongozi wa Kundi hilo, Corneille Nangaa.
Itakumbukwa, Nangaa alikuwa Kamishna wa Tume wa Uchaguzi wa mwaka 2018, wakati Rais Tshisekedi alipoingia madarakani akimpiku Kabila.
Ni baada ya kukorishana na Rais Tshisekedi mwaka 2021, ndipo Nangaa alipounda kikundi cha kuipinga Serikali, Alliance of the Congo River (ACF), ambacho baadaye kiliungana na wapiganaji wa M23.
Taarifa za Kabila kwenda katika Mji wa Goma, ambako ndiko M23 ilikokita mizizi, zilimchefua zaidi Rais Tshisekedi na ndipo alipoagiza mamlaka kukamata mali zake.
Itakumbukwa, M23 walithibitisha kuwa Kabila alifika Goma na kusema alikutana na viongozi wa dini na wakazi wa eneo hilo. Kabila alikanusha uhusiano wake na M23, ingawa alisema wana lengo moja; kuiondosha madarakani Serikali ya Rais Tshisekedi.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka wa mahakama ya kijeshi ya DRC, mmoja ya watu wa karibu wa Nangaa, Eric Nkuba, ameeleza kila kitu juu ya uhusiano wa Kabila na M23.
Nkuba, ambaye kwa sasa yuko gerezani, amesema Nangaa na Kabila walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na ajenda ni kumuondoa madarakani Rais Tshisekedi.
Hukumu ya kifo ina maana gani?
Mchambuzi wa masuala ya sheria mjini Goma, Nzanzu Masomeko Hubert, anasema hukumu ya kifo ya Kabila imetokana na sababu za kisiasa. Anasema hakuna ushahidi wa yale anayoshutumiwa kiongozi huyo na hukumu hiyo inaweza kuzalisha mapigano mapya na kufifisha jitihada za kurejesha amani nchini DRC.
“Naamini ni siasa tu. Kumshitaki na kumuhukumu Kabila wakati huu wa mazungumzo ya amani (kati ya Serikali na M23) ni kukosa dira. Ni kinyume cha kupigania umoja wa kitaifa, hasa kipindi hiki cha mgogoro,” anasema mchambuzi huyo.
Kwa upande wake, Kambale Musavuli, ambaye ni mtafiti wa DRC, anasema alichofanyiwa Kabila ni adhabu iliyokiuka misingi ya haki.
M23 waibuka, watoa tamko
Katibu Mkuu wa Chama chake cha PPRD, Emmanuel Ramazani Shadary, amelaani hukumu aliyopewa Kabila akiita kuwa ni matokeo ya siasa za chuki.
“Tunaamini lengo kuu la dikteta aliyeko madarakani (Rais Tshisekedi) ni kuondosha na kuwapunguza nguvu wakosoaji wake,” anasema Rais Shadary.
Pia, M23 kupitia kwa Msemaji wake, Bertrand Bisimwa, imemtaja Kabila kuwa ndiye rais na hukumu aliyopewa ni kinyume cha mazungumzo ya amani yaliyofanyika Doha, Qatar, kati yao na Serikali ya Rais Tshisekedi.
Published:


