6.4 C
New York

Usiyoyajua kuhusu penzi la Rotimi, Vanessa

Published:

LOS ANGELES, Marekani
ILIKUWA ni mwaka 2019, ndipo walipokutana kwa mara ya kwanza na hapo ukafunguliwa ukurasa mpya wa mapenzi kati yao.
Rotimi, ambaye ni mwanamuziki na mwigizaji wa Marekani mwenye asili ya Nigeria, na staa wa muziki wa Tanzania, Vanessa Mdee.
Kilichowakutanisha siku hiyo ni Tamasha la Utamaduni la Essence (Essence Festival of Culture) mjini New Orleans, Marekani, kila mmoja akifika hapo kwa ajili ya kutumbuiza.
“Nilipomuona, nikajisemea ‘huyu ndiye sahihi kwangu,” anasema Rotimi na kuongeza kuwa rafiki yake ndiye aliyemtambulisha kwa Vanessa na kuanzia hapo wakawa na stori nyingi.
Baada ya Tamasha hilo, licha ya Vanessa kurudi Tanzania na Rotimi kubaki zake Marekani, bado waliendelea kuwasiliana kwa stori za hapa na pale.
Haikuchukua muda mrefu, Vanessa alifunga safari hadi Marekani, lengo likiwa ni kumtembelea Rotimi. Kuanzia hapo, stori ikabadilika.
Urafiki huo wa karibu ulifuatiwa na ndoa iliyofungwa mwaka 2021 na sasa tayari mastaa hao wana watoto wawili.
Kwa mujibu wa Vanessa katika mahojiano na kituo cha runinga cha CNN, anasema Covid-19 ilikuwa na mchango mkubwa mno katika uhusiano wao.
Wakati huo, Vanessa alikwenda Marekani lakini akiwa anajiandaa kurudi Tanzania, ndipo zuio la kusafiri nje ya nchi lilipotangazwa na Marekani ikawa ndani ya karantini.
Kwamba sasa kipindi kile cha karantini (katazo la kutoka nje) kikawasaidia kukaa pamoja muda mrefu na kujuana zaidi.
“Kama ningewahi kidogo, basi ningerudi (Tanzania) tusingeonana kwa miezi kama tisa kutokana na zuio la kusafiri. Nashukuru Mungu kwa sababu alitutengenezea mazingira ya kujuana kwa ukaribu zaidi,” anasema.
Kama ilivyo kwa Vanessa, Rotimi naye anasema karantini ya Covid-19 ilikuja wakati mzuri kwake. “Mungu alitaka nitulie, nijifunze mambo mengi kuhusu huyu mwanamke,” anasema.
Katika mahojiano hayo na CNN, pia Vanessa amefichua kuwa alianza kuchomoza katika tasnia ya muziki akiwa na umri wa miaka 18.
Lakini pia, kupitia mahojiano hayo, Vanessa aliyewahi kuwa mmoja ya wasanii wakubwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, amezungumzia sababu ya kuachana na tasnia hiyo akiwa kwenye ubora mkubwa mwaka 2020.
“Kwa upande wangu, soko la muziki lilikuwa likiniathiri kiakili, kiimani, kihisia na kimwili kwa namna nyingi sana.
“Kuna namna haikuwa nzuri kwangu. Kuna kipindi soko la muziki lilikuwa hatari kwangu. Sisemi hii ni kwa kila mtu, ni kwa upande wangu,” anasema Vanessa.
Kwa sasa, Vanessa ni kiongozi wa ‘For The Better’, ambalo ni Jukwaa la kuwajenga watu, hasa wanawake, katika misingi ya Dini ya Ukiristo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img