11.6 C
New York

Simulizi ya kusikitisha maisha ya Gaza

Published:

LONDON, Uingereza
ACHANA na mashambulizi ya makombora yanayotupwa kila uchwao na Israel, raia wa Palestina walioko katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na shida nyingine kubwa inayoendelea kupunguza idadi yao kutokana na vifo.
Uhaba wa maji ya kunywa ni changamoto kubwa. Kwa mujibu wa wakazi wa Gaza, uhaba huo umeibua ugonjwa wa kipindupindu, huku wahanga wakubwa wakiwa ni watoto.
Wakati huo huo, uhaba wa maji safi si tu ni chanzo cha kipindupindu, bali pia umewasababishia watoto wengi magonjwa ya ngozi.
“Hakuna maji, watoto wetu wanateseka na magonjwa, hakuna hospitali na hakuna tiba,” anasema Akram Manasra (51), ambaye anaishi katika moja ya kambi zilizoko Gaza.
Manasra anaongeza kuwa tayari mabinti zake wadogo wawili wameathirika na hakuna uwezekano wa kuwapatia tiba.
“Tunajitahidi kufanya usafi, lakini siyo kwa kiwango cha kutosha kutokana na uhaba wa maji.
“Kutokana na uhaba wa maji, wakati mwingine kuoga ni changamoto. Tunajifuta kwa maji kama mbadala wa kuoga ili maji machache tunayopata yatoshe katika shughuli za kupika na kufua,” anasema Manasra.
Anasisitiza kuwa maji yanayotumika kufua ni yale yaliyobaki baada ya kuosha vyombo. “Hali ni mbaya, hairidhishi hata kidogo, inakufanya ukate tamaa.
“Unawezaje kuishi katika mazingira haya (ya uhaba wa maji) ukiwa na familia ya watu 10? Kuoga, kuosha vyombo na kufua,” anasema.
Naye mkewe, Umm Khaled, anafichua kuwa ni miezi mitatu sasa imepita bila familia hiyo kufua mashuka, licha ya kiwango cha juu cha joto huko Gaza.
Kwa upande mwingine, tatizo la uhaba wa maji safi katika maeneo ya Ukanda wa Gaza ni matokeo ya vita ya miezi 21 kati ya Israel na Palestina.
“Hatua ya Israel kusitisha misaada katika eneo hilo imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa majanga hayo kwa raia wasio na hatia, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake,” inaeleza ripoti ya mwezi huu ya Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA).
Mbaya zaidi, Israel imekuwa ikishambulia maeneo nyeti ya huduma za kijamii, jambo ambalo limeendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa Gaza.
Mathalan, mwishoni mwa wiki iliyopita, shambulizi lake liliua idadi kubwa ya watu waliokuwa kwenye foleni ya maji katika kambi ya wakimbikizi ya Nuseirat.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img