YAOUNDE, Cameroon
HATUA ya Rais wa Cameroon, Paul Biya, kutangaza nia ya kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu ujao imeonekana kuzua mjadala mkubwa katika siasa za Afrika.
Kwanza, ni umri mkubwa alionao kiongozi huyo. Biya wa Chama cha People’s Democratic Movement ana miaka 92 na ndiye Rais ‘mzee’ zaidi duniani.
Pili, ni muda mrefu aliokaa madarakani. Biya amekuwa Rais wa Taifa hilo tangu mwaka 1982. Kwamba anataka muhula wake wa nane, sawa na miaka 43, kwenye kiti cha urais.
Akizungumzia hatua yake ya kutaka kubaki Ikulu, Biya kupitia ukurasa wake wa ‘X’ (zamani Twitter), alisema ni ombi kutoka kwa wananchi wa mikoa yote ya Cameroon, pamoja na wale wanaishi nje ya nchi (diaspora).
Biya ameshindwa mara zote katika chaguzi alizowania tangu mwaka 1982 na endapo atashinda katika Uchaguzi wa Oktoba, basi atamaliza muhula wake wa nane akiwa anakaribia kutimiza umri wa miaka 100.
AMEFELI WAPI MIAKA 43 MADARAKANI?
Kwa miaka mingi, utawala wa Rais Biya umekuwa ukinyooshewa vidole katika maeneo mbalimbali.
Wakosoaji wake wamekuwa wakimpinga kwa shutuma za uongozi wake kutawaliwa na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa fedha za umma, pia hali mbaya ya usalama nchini humo.
Katika hoja nyingine, afya ya Rais Biya nayo imekuwa ikizua mijadala ya hapa na pale. Mathalan, mwaka jana, hakuonekana hadharani kwa wiki sita na hiyo ikaibua taarifa kuwa amefariki. Pia, kuna suala la maisha ya wananchi. Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa Pato la Taifa limeshuka kutoka asilimia 3.6 hadi asilimia 3.3.
Sambamba na hilo, bado asilimia 23 ya wananchi wa Cameroon wanasota katika umasikini wa kiwango cha kutisha.
Hiyo ni kando ya changamoto za miundombinuya usafiri, mawasiliano, achilia mbali Taifa hilo kutegemea zaidi uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hata hivyo, bado Rais Biya haoni kinachomnyima nafasi ya kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tena urais.
Akitangaza nia yake ya kugombea, alisema anajiona bado ana mengi ya kuwafanyia raia wa Cameroon katika kutimiza ndoto yao ya kutokomeza umasikini na changamoto zingine.
ATAFANIKIWA KURUDI IKULU?
Ukiweka kando ukosolewaji, Rais Biya anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa washirikia wake wa zamani wa Kaskazini mwa Cameroon.
Waziri Issa Tchiroma Bakary na aliyekuwa Waziri Mkuu, Bello Bouba Maigari, ambao walikuwa na mchango mkubwa wa kumtafutia kura katika eneo hilo, wamejitoa kwenye kambi yake na sasa kila mmoja anakitaka kiti cha urais.
Mwezi uliopita, kama itakumbukwa, Tchiroma alisema wazi kuwa uongozi wa Rais Biya umepoteza imani kwa wananchi wa Cameroon.
Wakati huo huo, pia Rais Biya anakabiliwa na upinzani imara kutoka kwa Maurice Kamto, ambaye alishika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018.
Licha ya Rais Biya kushinda kwa asilimia 71 ya kura, Uchaguzi huo ulikosolewa vikali, ikitajwa kutawaliwa na kasoro nyingi zilizolenga kumpa nafasi mkongwe huyo.
Mwaka mmoja baada ya Uchaguzi huo, Kamto alisoteshwa gerezani kwa miezi Ta tisa na hata kuachiwa kwake ni matokeo ya presha kubwa kutoka kwa jumuhiya za kimataifa, ikiwamo ‘G20’ (Muungano wa nchi tajiri 20 duniani).
Changamoto nyingine iliyo mbele ya Rais Biya ni Kanisa Katoliki, ambalo katika Mkutano wake wa 48 lilijadili pia siasa za Cameroon, ikiwa ni pamoja kuja na mapendekezo ya kumtaja kiongozi huyo kupisha wengine kwenye kiti cha urais.
WANANCHI WANASEMAJE?
Wakihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), wengi wameeleza kuhofia kutoa maoni yao hadharani, wakihofia kufikiwa na mkono wa vyombo vya dola.
Hata waliothubutu kutoa maoni yao mbele ya mwandishi wa habari wa BBC, bado hawakuwa huru kutaka majina, umri au kazi zao.
“Sijawahi kuona wala kusikia kokote pale, Rais mwenye umri ule anatangaza kugombea katika Uchaguzi. Nafikiri angeondoka na kwenda kupumzika na kupisha kizazi kipya,” anasema mmoja ya wakazi wa Yaounde, Camille Esselem.
Lakini, wapo baadhi ya raia wa Cameroon wanaokubaliana na uamuzi wa Rais Biya kugombea tena, wakiamini mwanasiasa huyo bado anatosha.
“Bado Rais ana mengi ya kuwafanyia watu wa Cameroon,” anasema Ngono Marius, ambaye hata hivyo ni mtumishi wa Serikali.
Kwa upande wake, Marius hatofautiani na Sylvia Tipa, anayesema haoni kama kuna mpinzani wa kumzidi Rais Biya.
“Ameifanyia makubwa sana nchi hii. Tumeona kazi yake katika kushughulikia migogoro na mengi aliyofanya,” anasisitiza Tipa.
Published:


