11.6 C
New York

Kundi la kigaidi linaloitesa Afrika Magharibi

Published:

BAMAKO, Mali
KWA miaka ya hivi karibuni, Ukanda wa Afrika Magharibi umekuwa ukiandamwa na mashambulizi ya kigaidi yanayotekelezwa na Kundi la Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) linalotajwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Al-Qaeda.
JNIM limekuwa likifanya mashambulizi yake mengi na kwa nyakati tofauti katika mataifa ya Burkina Faso, Mali na Niger.
Mwanzoni mwa mwezi huu (Julai Mosi, 2025), JNIM lilikiri kuhusika katika mashambulizi ya kujitoa muhanga huko Magharibi mwa Mali, ikiwamo maeneo ya jirani na mpaka wa Senegal na Mauritania.
Kufikia Juni, mwaka huu, JNIM lilishatekeleza mashambulizi 280 nchini Burkina Faso. Idadi hiyo ni mara mbili ya yaliyoripotiwa mwaka jana.
Kundi hilo liliweka wazi pia, kwamba mashambulizi yake yameua watu 1000, wengi wao wakiwa ni wanajeshi wa kigeni wanaozisaidia Serikali za Afrika Magharibi.
Je, JNIM limetokea wapi? Kwa historia yake ufupi, hilo ni Kundi lililoasisiwa mwaka 2017.
Ifahamike kuwa Kundi hilo ni matokeo ya muungano wa vikundi vya kigaidi lilivyokuwa vikijitanabaisha kufuata misimamo mikali na sheria za Dini ya Uislam.
Aidha, kuzaliwa kwa JNIM kulikuja baada ya wanajeshi wa Ufaransa kusambaratisha vikundi vidogo vya kigaidi vilivyokuwa vimeota mizizi Kaskazini mwa Mali.
Ni baada ya kuzidiwa nguvu na operesheni za Ufaransa mwaka 2012, ndipo viongozi wa vikundi hivyo walipoungana na kuasisi JNIM.
Nani kiongozi wa Kundi hilo? Kwa sasa, kiongozi mkuu wa JNIM ni aliyekuwa mwanadiplomasia mahiri wa Mali, Iyad Ag Ghali, ambaye anatokea Kabila la Tuareg.
Kama itakumbukwa, Ghali ndiye aliyekuwa kiongozi wa Tuareg wakati wa vuguvugu la kuipinga Serikali ya Mali mwaka 2012.
Katika majukumu yake ndani ya Kundi la JNIM, msaidizi wake ni Amadou Koufa anayetokea Kabila la Fulani.
Licha ya kwamba haijafahamika idadi kamili ya wapiganaji ilionao, JNIM inaaminika kuwa na jeshi lenye vijana, wengi wao wakiwa ni wale wanaotokea katika familia zisizojiweza kiuchumi.
Ripoti zinaeleza kuwa kwa miaka ya hivi karibuni, Kundi hilo limejitanua na kushika maeneo mengi zaidi ya Magharibi mwa Afrika.
Mathalan, ukiacha Mali, Burkina Faso na Niger, pia Kundi hilo limejisogeza na kuweka alama zake katika mataifa ya Benin, Togo na hata Ivory Coast.
Kuthibitisha ukubwa wake, utafiti wa Taasisi ya Kupinga Uhalifu ya Gi-Toc, unaonesha kuwa JNIM inafanya shughuli zake katika miji 11 kati ya 13 ya Burkina Faso.
“Takwimu za matukio ya JNIM ziko wazi kuwa kwa mwaka jana pekee, Burkina Faso ndiyo nchi iliyothirika zaidi,” anasema mchambuzi wa masuala ya usalama wa Taasisi ya Control Risk, Beverly Ochieng.
Kwa mujibu wa Ochieng, hiyo ilitokana na mpasuko mkubwa uliokuwepo ndani ya jeshi la nchi hiyo, hivyo kuathiri hali ya usalama katika mipaka ya Taifa hilo.
Lengo la JNIM ni nini? Kundi hilo linapinga Serikali zote zilizopo Afrika Magharibi, likidai kuwa viongozi waliopo madarakani wameshindwa kuwapa haki ya maisha bora wananchi wake.
Pia, matamanio ya JNIM ni kuona sheria za Uislam (Sharia) zikitumika kuongoza katika mataifa ya Ukanda huo.
Ni katika hilo, tayari JNIM imeshasimika na kusimamia kwa nguvu kubwa ‘Sharia’ katika maeneo mbalimbali, ikiwamo kupiga marufuku usikilizaji wa muziki na uvutaji wa sigara.
Pia, yameripotiwa matukio ya kulazimisha wanaume kufuga ndevu na kuzuia wanawake kuonekana katika maeneo ya wazi.
Je, JNIM ina nguvu ya kiuchumi kiasi gani? Kwamba linawezaje kujiendesha? Kama zilivyo taasisi zingine, Kundi hilo lina vyanzo vyake vya mapato.
Wakati fulani, lilikuwa na utamaduni wa kuwateka raia wa kigeni na kushinikiza wapewe pesa ili kuwaachia.
“Hata hivyo, kwa sasa, JNIM limekuwa likitekeleza operesheni ya kuteka mifugo, hasa ng’ombe wanaosafirishwa nje ya nchi.
“Mali ni moja ya mataifa yenye kiwango kikubwa cha usafirishaji wa mifugo. Hivyo, kwa JNIM, hii ni njia rahisi zaidi kwao kuiba na kuuza,” inaeleza taarifa ya Taasisi ya Gi-Toc.
Ripoti ya utafiti ya Taasisi hiyo inaonesha kuwa kwa mwaka mmoja, JNIM inaingiza si chini ya Dola za Marekani 770,000 kutokana na wizi wa mifugo nchini Mali.
“Vilevile, huwa wanatoza kodi kwenye madini na chochote kinachopita kwenye eneo lao. Pia, wamekuwa wakiwatoza kodi wananchi kwa madai ya kuwawekea ulinzi,” inaeleza taarifa ya uchunguzi ya Gi-Toc.
Je, ni rahisi kiasi gani kuliondosha Kundi hilo katika Ukanda wa Afrika Magharibi?
Wanajeshi wa Ufaransa zaidi ya 4000 walikuwa nchini Mali kwa miaka takribani 10, wakipambana na vikundi vya kigaidi.
Ikumbukwe, kati ya mwaka 2013 na 2014, Ufaransa ilionekana kupata mafanikio baada ya kukomboa maeneo yaliyokuwa chini ya vikundi hivyo.
Lakini, jitihada hizo hazikumaliza tatizo na badala yake ikazaliwa JNIM, ambayo imeonekana kuwa tishio zaidi, labda kuliko vikundi vilivyokuwepo awali.
Mwaka 2014, viongozi wa Afrika Magharibi waliungana na kuasisi mpango-kazi wa kulishughulikia na kulitokomeza Kundi la JNIM.
Lakini, Umoja huo ulipachikwa jina la ‘G5 Sahel Task Force’ haukupiga hatua ya maana katika kukabiliana na JNIM.
Mbaya zaidi, haikuchukua muda mrefu kabla ya kuziona Burkina Faso, Mali na Niger zikijitoa.
Kama hiyo haitoshi, mwaka jana, Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Minusma) lililokuwa Mali kwa miaka 10, nalo lilijiondoa.
Ni kutokana na mazingira hayo, ndipo ripoti ya Gi-Toc inapoeleza kuwa njia pekee iliyobaki ya kuizima JNIM siyo tena uwanja wa vita, bali meza ya mazungumzo ya kutafuta suluhu kati ya Kundi hilo na viongozi wa Serikali za Afrika Magharibi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img