9.8 C
New York

Ruto atafaulu mtihani wa ‘Gen Z’?

Published:

NAIROBI, Kenya
UPEPO unavuma vibaya kwa William Ruto, huku sehemu kubwa ya wakosoaji wake wakiwa ni vijana wa kizazi kipya, wakifahamika pia kwa jina la ‘Gen Z’ (Generation Z).
Kwao, Ruto ni Rais ‘kimeo’ zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Wakosoaji wake wanasema kiongozi huyo ameshindwa kutekeleza ahadi ya maisha bora aliyowaahidi wakati wa kampeni za kuomba ridhaa ya kuingia madarakani.
Tujikumbushe; wakati wa kampeni zake za kuwania urais, Ruto alipata uungwaji mkono mkubwa wa vijana, hasa kwa namna alivyojitanabaisha kuwa ni ‘mtoto wa mkulima’.
Historia ilimbeba. Ni kweli ametokea katika maisha ya ‘kuungaunga’, wakati fulani akilazimika kuuza kuku ili kumudu gharama za maisha.
Hata hivyo, kupingwa kwa utawala wa Rais Ruto kulianza mwaka mmoja tu baada ya mwanasiasa huyo kuingia Ikulu.
Kwa takwinu za mwaka mmoja tu, tayari watu zaidi ya 100, wakiwamo vijana waliompigia kura, wameshapoteza maisha katika maandamano ya kupinga uongozi wake.
Hivi karibuni, akionesha kuvurugwa na hali ya mambo, hasa maandamano yanayoendelea, Rais Ruto aliuliza sababu ya utawala wake kukosolewa vikali kuliko marais wengine waliowahi kuiongoza Kenya.
Rais Ruto aliutolea mfano utawala wa miaka zaidi ya 20 wa Daniel arap Moi, ambaye aliiongoza kwa ‘mkono wa chuma’ na kusigina haki za binadamu.
Hoja yake ikawa hivi; kwanini anachukiwa kuliko Moi, wakati mtangulizi wake huyo alikuwa na utawala wa kidikteta?
Wakati huu ukosoaji ukiwa wa kiwango cha juu dhidi ya Rais Ruto, suala la ukabila limechomoza kwa kasi.
Kikuyu ni moja ya makabila makubwa na lilikuwa na mchango mkubwa kwa Ruto katika ushindi wake wa kuingia madarakani mwaka 2022.
Sasa, baada ya Rais Ruto ‘kumtumbua’ Naibu wake, Rigathi Gachagua, ambaye anatokea Kabila hilo, nao wameamua kugeuka na kuwa wapinzani wa Serikali iliyoko madarakani.
Lakini, kwa mtazamo wa mchambuzi wa siasa, Mark Bichachi, mambo hayako hivyo.
Kwa upande wake, Bichachi anaamini ukabila hauna nafasi katika hiki kinachomkuta Rais Ruto, na badala yake ni matokeo ya wananchi kutokuona kiongozi huyo akitimiza ahadi alizoweka, ikiwamo ya kupunguza ukali wa maisha.
Msomi mwingine, Dk. Njoki Wamai, anasema kinachomkuta Rais Ruto si kigeni katika siasa za Kenya.
“Marais wote walikumbana na mazingira ya kukosolewa pale walipovunja Katiba au kwenda kinyume na matakwa ya Wakenya,” anasema.
Dk. Wamai anaenda mbali zaidi na kutolea mfano utawala wa Moi, ambao ulikaribia kupinduliwa mwaka 1982.
“Tofauti iliyopo ni kwamba sasa kuna kasi kubwa ya upashanaji wa habari,” anasema Dk. Wamai akitokea mfano uwepo wa mitandao ya kijamii inayowaleta pamoja vijana katika kujadili ajenda za kitaifa.
Kupitia majukwa ya kidigitali, vijana wamekuwa wakiendesha kampeni za kupinga ugumu wa maisha, utitiri wa kodi, rushwa, achilia mbali nguvu kubwa wanayotumia polisi dhidi ya wakosoaji.
Anaongeza kuwa changamoto kubwa inayomkabili Rais Ruto ni uhafidhina, hivyo kushindwa kwenda sambamba na maono ya vijana wa kiazi cha sasa.
Hata hivyo, kwa upande wake, bado Rais Ruto anaamini Serikali yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kukimbizana na changamoto za kimaisha zinazowakabili Wakenya.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img