Na mwandishi wetu, Gazetini
KLABU ya Yanga imemtangaza Pedro Goncalves kuwa kocha wake mpya na Mreno huyo anachukua mikoba ya Romain Folz aliyetimuliwa siku chache zilizopita.
Goncalves ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Angola na makala haya yanakuibulia mambo 10 kuhusu kocha huyo. Ni nani huyo? Endelea kusoma.
Alipita Sporting Lisbon
Alizaliwa Februari 7, 1976, mjini Lisbon. Alianza kazi ya ukocha mwaka 1997 akiwa msaidizi katika benchi la ufundi la klabu ya Amora FC.
Baadaye, Goncalves alijiunga na Cova da Piedade, kabla ya kuajiriwa na klabu kongwe ya Sporting Lisbon kwa ajili ya kuwa skauti na kisha kukabidhiwa jukumu la kuzinoa timu za vijana.
Rekodi za kutisha Angola
Alitua Afrika mwaka 2025, akianzia katika timu za vijana za U-17, U-20 na U-23 za klabu kubwa nchini humo, Primeiro de Agosto.
Akiwa na U-17, Goncalves alitwaa ubingwa wa COSAFA na kubeba medali ya shaba katika michuano ya AFCON ya vijana.
Ikumbukwe, pia alipokuwa mkuu wa benchi la ufundi la vijana wa U-19, Angola ilifuzu kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Dunia.
Mafanikio hayo yalimpa ajira ya kuinoa timu ya taifa ya Angola mwaka 2019. Aliiwezesha kufuzu na kuonesha kiwango kizuri katika michuano ya CHAN (2022) na kufika robo fainali ya AFCON (2023).
Kwa miaka sita akiwa kocha, aliweka rekodi ya kuwa kocha aliyeshinda mechi nyingi (24), pia mwaka jana alitwaa ubingwa wa COSAFA kwa kuifunga Namibia na mabao 5-0 katika mchezo wa fainali.
Aishangaza Ghana, aandika historia
Ilikuwa ni Septemba 5, mwaka jana, ambapo Angola ilikuwa ugenini kucheza na vigogo wa soka la Afrika Magharibi, Ghana ‘Black Stars’.
Chini ya Goncalves, Angola iliibuka na ushindi wa bao 1-0, hivyo kumaliza ubabe wa Ghana, ambayo haikuwa imefungwa katika mechi 24 mfululizo za mashindano ikiwa nyumbani.
Kaizer Chiefs, Al Ahly zilimgombea
Kwa namna alivyokuwa kwenye rada za klabu nyingi na kubwa barani Afrika, Yanga wana bahati kuinasa saini ya Goncalves kipindi hiki.
Siku mbili tu baada ya Kaizer Chiefs kutangaza kumfuta kazi Nasreddine Nabi, klabu hiyo ya Afrika Kusini ilihusishwa na Goncalves. Pia, vigogo wa Ligi Kuu ya Misri, Al Ahly, nao walitajwa kumpigia hesabu kocha huyo.
Mtihani unaomsubiri Jangwani
Goncalves aliyeachana na timu ya taifa ya Angola mwezi uliopita, ana kibarua cha kuivusha Yanga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Yanga ilitinga makundi baada ya ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Silver Strikers. Mchezo wa kwanza ulichezwa Malawi na Yanga kufungwa bao 1-0, kabla ya ‘kupindua meza’
Wakati huo huo, changamoto nyingine aliyonayo kocha huyo ni kulibakiza Jangwani taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, ambalo Yanga wamelibeba mara nne mfululizo (2021–22, 2022–23, 2023–24, 2024–25).
Published:


