15.5 C
New York

Nini kifanyike kuiokoa Sudan?

Published:

DARFUR, Sudan
WATU takribani 300,000 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula ukiwa ni mwaka mmoja tu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan. Hali ni mbaya zaidi katika Mji wa El Fasher, ambao kwa mwaka mmoja sasa umegeuka uwanja wa vita.
“Jitihada za Umoja wa Mataifa (UN) zimeonekana kugonga mwamba kwani wapiganaji wamezuia barabara zote zilizokuwa zikitumika kupeleka misaada kwa ya chakula,” inaeleza taarifa ya Programu ya Chakula ya UN (WFP).
Kupitia taarifa yao ya hivi karibuni, WFP inaongeza kuwa wakazi wa El Fasher wanapata vyakula kwa bei kubwa, ukilinganisha na wenzao wa maeneo yote nchini Sudan.
Achilia mbali 16,000 waliopoteza maisha, takribani watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao nchini Sudan na kwa ttafsiri ya UN, kinachoendelea ni majanga makubwa zaidi ya kibinadamu kuwahi kutokea duniani.
CHANZO CHA VITA
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya vikundi viwili vya kijeshi kugombea utawala. Vikundi hivyo ni Rapid Support Forces (RSF) na Sudanese Armed Forces (SAF).
Ikumbukwe, chanzo ni kushindwa kukubaliana juu ya kundi lipi liingie madarakani kuiongoza Sudan baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.
SAF ni jeshi la Serikali chini ya Rais Abdel-Fattah Burhan, likitajwa kuwa na wapiganaji takribani 200,000. Ifahamike kuwa jeshi hilo ndilo linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Kwa upande wake, RSF lenye wapiganaji wanaofikia 100,000, linaongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, wengi wakimfahamu kwa jina la Hemedti. Ni jeshi lenye wapiganaji wa Janjaweed, ambao walitikisa kwa mashambulizi yao nchini Sudan mwanzoni mwa miaka ya 2000.
El Fasher umebaki kuwa ndiyo mji pekee wa Magharibi mwa Sudan, ambao hauko chini ya wapiganaji wa RSF. Kwamba endapo watafanikiwa, basi Kundi hilo litakuwa limeiteka sehemu kubwa ya eneo hilo la Magharibi, wakati SAF wanaendelea kushikilia upande wa Kaskazini.
Wakati huo huo, yapo madai kuwa mgogoro wa RSF na SAF umekuwa ukichangiwa na mataifa ya nje. Kwamba Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimekuwa zikifadhili makundi hayo. Licha ya kukana, Misri na Saudia zinatajwa kuwa upande wa SAF, wakati UAE iko na RSF.
MASILAHI BINAFSI, NINI KIFANYIKE?
Akihojiwa na VOA, Msemaji wa watu waliokimbia makazi yao kutokana na mgogoro huo, Adam Roja, kinachoendelea sasa kati ya RSF na SAF ni matokeo ya kugombea masilahi binafsi.
“Hakuna suala la uzalendo. Wanapigania masilahi yao, inayoumia ni jamii ya Wasudan. Watu wamepoteza kila kitu,” anasema Roja na kusisitiza kuwa maneno hayatoshi kuzungumzia hali mbaya iliyopo Sudan.
Siku chache zilizopita, Katika Mkuu wa UN, Antonio Guterres, alijitokeza akiyaomba makundi hayo, SAF na RSF, kusitisha vita walau kwa wiki moja ili misaada iingie na kuwafikia wakazi wa El Fasher.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wachambuzi, jumuhiya za kimataifa hazijafanya vya kutosha kumaliza mgogoro wa Sudan. Mtaalamu wa masuala ya majanga, Alan Boswell, anazungumzia hilo akisema:
“Unaweza kuona namna jumuhiya za kimataifa zilivyoelekeza nguvu kubwa katika migogoro ya Gaza na Ukraine. Fikiria tu, vipi kama ingetumika asilimia tano tu ya nguvu hizo kwa Sudan. Ingeokoa maisha ya watu wangapi?”
Pia, sababu za kiuchumi nazo zimetajwa. Kwamba mataifa ya Magharibi hayaoni sababu ya kuingilia kinachoendelea Sudan kwa kuwa haina masilahi ya moja kwa moja ya kibiashara na Taifa hilo la Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img