15.5 C
New York

Huyu ndiye mwandishi aliyeuawa, aliyeacha simanzi Gaza

Published:

JERUSALEM, Palestina
SIKU chache zilizopita, tukio la mauaji ya waandishi wa habari watano huko Gaza lilitikisa ulimwengu, huku Israel ikifahamika kuwa ndiyo iliyohusika kupitia mashambulizi yake katika Ukanda huo wenye Wapalestina wengi.
Mmoja ya waandishi hao ni Anas al-Sharif wa kituo cha Al Jazeera, ambaye mvuto wake mkubwa mbele ya Wapalestina kutokana na namna aliyokuwa akiripoti mateso wanayopitia kutokana na mashambulizi ya Israel.
“Alifanya kazi kwa kipindi kirefu cha vita, akiripoti matukio ya kila siku na hali inavyoendelea wakati wa mashambulizi huko Gaza,” anasema Mkurugenzi wa Al Jazeera, Salah Negm.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Mohamed Moawad, anamtaja Al-Sharif kuwa ni ‘sauti pekee ya watu wa Gaza iliyokuwa imebaki wakati huu wa vita’.
KWANINI ADUI WA ISRAEL?
Kabla ya shambulizi lililomuua Al-Sharif na wenzake wanne, Israel ilikuwa ikimtaja mwandishi huyo kuwa ni mshirika wa Kundi la wapiganaji wa Palestina, Hamas, ingawa haikuwahi kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
Wakati fulani, Israel ilidai kuwa ilikuwa na nyaraka zinazoonesha mafunzo, ratiba ya kazi na hata mshahara wa mwandishi huyo ndani ya Hamas.
Lakini, ni madai ambayo yalikuwa yakipingwa vikali na kituo chake cha kazi, Al Jazeera, pamoja na taasisi za kimataifa zinazopigania haki za waandishi wa habari.
Wakati huo huo, tofauti na madai ya Israel, Al-Sharif kupitia mitandao ya kijamii, alikuwa mkosoaji mzuri wa kile kinachofanywa na Kundi la Hamas.
Mtendaji Mkuu wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi (CPJ), Jodie Ginsberg, anasema: “Israel haijawahi kuja na ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha madai hayo (dhidi ya Al-Sharif).
BABA YAKE ALIUAWA
Mwishoni mwa mwaka 2023, Al-Sharif mzaliwa wa mjini Jabalia, alimpoteza baba yake katikati ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Mwaka jana, mwandishi huyo aliripoti juu ya kuuawa kwa wenzake wawili wa Al Jazeera, Ismail al-Ghoul na Rami al-Rifi, ambao nao walipotezwa na shambulizi la anga la Israel.
Kwa upande wake, Al-Sharif ameondoka katika uso wa dunia akiwa ameacha mke na watoto wawili, akiwamo mdogo wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja.
“Moyo wake wa kujitoa ulimfanya aiache familia yake kwa miezi kadhaa ya vita na afike katika maeneo, ambayo hakuna mwandishi angethubutu kufika kutokana na mauaji yaliyokuwa yanaendelea,” anasema Raed Fakih, Meneja wa Al Jazeera kwa upande wa lugha ya Kiarabu.
Fakih anaongeza: “Katika mazungumzo yetu ya mwisho kwa njia ya simu, alinambia alivyokuwa akipitia changamoto ya njaa, namna ilivyokuwa ngumu kuishi kwa chakula kidogo.
“Kwake, alijiona hana cha kufanya zaidi ya kuwa sauti ya wanyonge wa Gaza. (Akiwa huko), aliishi maisha magumu kama watu wengine, njaa na kuomboleza vifo vya raia.”
MWENDELEZO WA ISRAEL KUUA WAANDISHI?
Kuziweka sawa takwimu, mashambulizi ya Israel yameshagharimu maisha ya waandishi takribani 200 katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba, 2023.
Wanaharakati wanaamini Israel inafanya hivyo ili kuzuia kuvuja kwa taarifa za ukatili inaofanya dhidi ya Wapalestina. Israel imekuwa ikikana shutuma hizo.
Itakumbukwa, mwandishi mkongwe raia wa Palestina, Shireen Abu Aqla, alipigwa risasi ya kichwa wakati Israel ikilichukua eneo la West Bank mwaka 2022.
Katika utetezi, Israel ilidai kuwa mwanajeshi wake alimuua bila kukusudia, ingawa Al Jazeera ilisema ulikuwa ni mpango uliosukwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img