Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema katika kuimarisha sekta ya hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha kuratibu kaboni, imesajili jumla ya miradi 73 ya biashara ya kaboni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Waziri Masauni ameyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026.

Amesema biashara ya kaboni imeanza kuleta manufaa kiasi katika baadhi ya maeneo nchini ambapo kiasi cha Sh 45 bilioni zimelipwa na kunufaisha wananchi katika Halmashauri 10 nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni.
“Ofisi iliratibu vikao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao cha kuwajengea uwezo Makatibu Wakuu 21 kuhusu biashara ya kaboni, wawakilishi wa wakampuni 27 yanayojihusisha na biashara ya kaboni,vikao vya kimkakati vya kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara za kisekta” amesema Waziri Masauni.
Aidha amesema kuwa katika mwaka 2024/2025 Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano (UNUMMiS).
Waziri Masauni amesema mfumo huo umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na utendaji kazi
Amesema mfumo huo kwa sasa upo katika hatua za majaribio ili kuona kama unakidhi matakwa ya watumiaji na pindi utakapokamilika utasaidia wananchi kufahamu kwa kina masuala muhimu yanayohusu Muungano.
Ameeleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha wizara/idara na taasisi zinafanya vikao vya ushirikiano.
Ameongeza kuwa hadi kufikia Machi 2025 jumla ya vikao vinane vya ushirikiano vilifanyika vilivyolenga katika kubadilishana uzoefu, Sera, Sheria na utaalamu katika utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano.
Kuhusu uchumi wa Buluu, Waziri Masauni amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu utekelezaji wa sera ya taifa ya uchumi wa buluu ikiwemo kuandaa Mpango wa Matumizi wa Maeneo ya Maji pamoja na kuwezesha uwepo wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu nchini.
Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191, Mhandisi Masuani amesema hadi kufikia machi 2025, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilipokea na kushughulikia malalamiko 247 yaliyohusu kelele, utupaji taka ovyo, utiririshaji ovyo wa majitaka, ujenzi holela, uchimbaji usio rasmi wa mchanga na uchafuzi wa hewa.