*Mtaalam aeleza vinavyosababisha mtindio wa ubongo kwa watoto
Na Faraja Masinde, Gazetini
Kundi la Wanawake na Watoto limetajwa kuwa hatarini zaidi kuathirika na matumizi ya viuatilifu ambavyo vimekuwa vikiingia nchini kutoka nje ya nchi huku vingine vikipitia njia zisizo rasmi kutokana na kushindwa kukidhi ubora.
Hayo yamebainishwa Dar es Salaam leo Machi 6, 2024 na Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya na Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Vera Ngowi, wakati wa warsha ya Kutathmini shughuli zilizofanywa na Mtandao wa Asasi zisizokuwa za kiserikali Tanzania katika kuondoa viuatilifu chakavu barani Afrika iliyoandaliwa na Asasi ya AGENDA kwa kushirikiana na TAPOHE.
Amesema wanawake na watoto wako katika hatari ya kupata madhara ya viutilifu kwa afya kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika nchini kuonyesha hivyo.
“Mara nyingi wanawake wanajiona kwamba wao ni salama kwa kuwa tu hawabebi mabomba kwenda kupulizia viuatilifu shambani au majumbani, lakini tafiti ambazo zimefanyika katika nchi mbalimbali ikiwamo hapa Tanzania tumeona kwamba wanawake wanaathirika zaidi na viuatilifu hivi kuliko wanaume wanaobeba mabomba kwenda kupulizia mazao.
“Hii inatokana kwamba wanaume wanakuwa wamechukua tahadhari kwa kujikinga kisha baada ya kukamilisha kazi yao wanarudi nyumbani na kuoga, changamoto inakuja kwa wanawake ambao wanachukua nguo hizo ambazo tayari zina viuatilifu na kuzifua bila kuchukua tahadhari hatua inayosababisha kunasa viuatilifu hizo kwa njia ya ngozi,” amesema Dk. Vera na kuongeza kuwa:
“Pia utaona kuwa wanawake hawa ndio wanakuwa na jukumu la kurudi shambani kwa ajili ya kupalilia mazao au kuvuna, sasa mama anapoathirika ni mtoto pia ameathirika sababu wanaenda na watoto shambani na kemikali hizo iwapo mama atakuwa mjamzito zitaenda moja kwa moja kwa mtoto au hata baadae akija kupata ujauzito madhara yataonekana kwa mtoto atakayezaliwa,” amesema Dk. Vera.
Kulingana na mtaalamu huyo, athari za kemikali hizo zinazotokana na viuatilifu ni pamoja na kuzaa mtoto mwenye mtindio wa ubongo, saratani, mtoto asiye na utulivu na madhara mengine.
Kulingana na Dk. Vera, madhara ya viuatilifu hasa vile bandia au vilivyoisha muda wake kwa wanawake ni mara nne zaidi ikilinganishwa na wanaume huku akisema kuwa jamii hususan wakulima wanapaswa kuelimishwa na kutambua kuwa viuatilifu ni hatari.
“Tunatamani watu watambue kuwa kuna viuatilifu vilivyoisha muda wake ambavyo vinauzwa katika maduka ya pembejeo, wakulima nao hawajui sababu wanataka kupata mazao mengi na bora bila kujali athari zake baadae.
“Tunaendelea kusisitiza elimu zaidi kwa jamii ili watambue kuwa viuatilifu ni hatari…ni hatari kwa wote ila mwanamke anaathirika tu sababu ya maumbile yake na shughuli za kila siku.
“Ushauri kwa wakulima angalia kama huna ulazima wa kupuliza viuatilifu usifanye hivyo, hata wale wa majumbani wanaopuliza kwa Sh 2,000 wengi wanapuliza viuatilifu vilivyoisha muda wake ,” amesema Dk. Vera.
Amesema ni vyema Serikali hususan Wizara zinazohusika ikiwamo ile ya Kilimo kuangalia namna ya kudhibiti viuatilifu ambavyo vimekuwa vikiingia nchini.
Awali, Afisa Program Mkuu wa Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya Mazingira na Maendeleo, Silvani Mng’anya, kumekuwa na matumizi yasiyo ya lazima ya viuatilifu nchini hususan katika nyanja ya kilimo hatua ambayo inachochea madhara zaidi ya kiafya kwa binadamu.
“Kumekuwa na madhara mengi katika matumizi ya viuatilifu yasiyo sahihi na ya lazima hasa ambavyo vimeisha muda wake na kwa sehemu kubwa vimekuwa vikitumika katika kilimo hapa nchini.
“Wananchi wengi wanatumia viuatilifu bila kuwa na elimu matokeo yake vinakuja kuleta madhara baadae, kwa hapa nchini ukiangalia hali bado haridhishi kwani uelewa uko chini na baadhi ya maeneo wanatumia viuatilifu zaidi ya kimoja kwenye ndoo moja matokeo yake mazao anayopulizia yanaenda kuleta madhara kwa mlaji ikiwamo kuathiri mazingira, hivyo matumizi ya viuatilifu bado siyo mazuri nchini,” amesema Mng’anya.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani(WHO) ya mwaka 2010 ilikadiria kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo yale yanayosababishwa na viuatilifu yatasababisha vifo Barani Afrika kuliko magonjwa ya kuambukiza na ya lishe ikiwamo vifo vya mama na watoto kwa pamoja ifikapo mwaka 2030.
Akitoa ushauri kwa wanawake juu ya kupulizia dawa ndani, Katibu Mtendaji wa AGENDA, Dorah Swai, amesela ni vema wanawake wakaelimishwa juu ya madhara hayo.
“Ushauri kuhusu kupiga dawa ndani, wanawake waambiewe kabisa madhara ya viautilifu, kwani tunafahamu kuwa madhara yake kwa watoto ni makubwa zaidi kuliko inavyochukuliwa,” amesema Dorah.
Akizungumzia changamoto hiyo ya viuatilifu, Wakili Kitua Kinja kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo Tanzania(TPAWU) amesema sheria pia bado ni changamoto, kwani haiwawajibishi watu wanaofanya kazi ya kuuza viuatilifu hasa vile ambavyo ni bandia.
“Madhara yatokanayo na matumizi ya viuatilifu ni mengi na hii inasababishwa kwamba bado sheria haiwabani watu wanaoingia bidhaa hizi hasa zile bandia, kwani sumu zinapoingia mwilini zinaenda kuharibu mifumo ya neva, ukiangalia mfano kijijini bado elimu haijafika juu ya matumizi ya viuatilifu.
“Wananchi wengi hawana uelewa, mkulima anajua tu kwamba hii ni dawa naenda kupuliza kwenye shashmani kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia mazao bila kuwa na elimu. Hivyo, kama wadau tunalo jukumu la kuendelea kuishinikiza Serikali ili iweze kuchukua hatua ikiwamo kuangalia tena sheria,” amesema Wakili Kinja.
Serikali na udhibiti wa Viuatilifu bandia
Katika kukabiliana na changamoto ya viuatilifu bandia, Machi mosi, 2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) ilisema kuwa inatarajia kuanzisha maabara ndogo kwenye vituo 17 vya ukaguzi mipakani.
Hatua hiyo ilikuja kufuatia mamlaka hiyo kudai bado kuna changamoto ya viatilifu bandia kuingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na njia za panya.