6.6 C
New York

Samia agawa wizara mbili, afanya mabadiliko ya viongozi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-DAR

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko ya muundo wa wizara mbili, uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali wa Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji wa Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 25, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yanahusisha kugawanywa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuanzishwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawanywa na kuwa Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uvuvi.

Katika mabadiliko hayo, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akitokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Angellah Kairuki ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akitokea Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Balozi Dk. Bashiru Ally ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo, akitoka katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, huku Hamis Mohamed Mwinjuma akiteuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi, akitokea Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Vilevile, David Silinde ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akitokea Naibu Waziri wa Kilimo, wakati Beng’i Mazana Issa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Naibu mawaziri

Katika ngazi ya naibu mawaziri, Dk. Ngwaru Maghembe ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku James Millya akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ng’wasi Damas Kamani ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo, Subira Mgalu kuwa Naibu Waziri wa Uvuvi na Cecilia Paresso kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Mabadiliko ya makatibu wakuu

Kwa upande wa makatibu wakuu, Agnes Meena ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, huku Profesa Mohammed Ali Sheikh akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi.

Eliakim Maswi amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Gerson Msigwa amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Aidha, Abdallah Mitawi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akitokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.

Katika mgawanyo wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Dk. Samwel Shelukindo amepangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Charles Ngeleja Kadonya akipangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Naibu makatibu wakuu na nafasi nyingine

Balozi Said Mussa amepangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Dk. Fabian Madele akipangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo.

Dadi Horace Kolimba ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi, akitokea nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Wakati huohuo, Elijah Mwandumbya amehamishwa kutoka Wizara ya Fedha kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, huku Dk. Amos Ibrahim akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia masuala ya usimamizi wa uchumi.

Katika nafasi nyingine, Dk. Ayub Rioba Chacha ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Balozi Meja Jenerali Wilbert Augustin Ibuge amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, akitokea nafasi ya Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).

Mhandisi Gilbert Godfried Mwoga ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), akichukua nafasi ya Mhandisi Victor Hudson Seff ambaye amemaliza muda wake. Kabla ya uteuzi huo, Mwoga alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Miundombinu katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Pia, Katibu Mkuu Mstaafu Adolf Ndunguru ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), akichukua nafasi ya Zakhia Hamdani Meghji ambaye amemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, uapisho wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wateule utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.

Related articles

Recent articles