Na Hassan Mwasha, Gazetini – DAR
KIPINDI hicho! Hamis Mohamed Mwinjuma halikuwa jina lenye nafasi yoyote kwenye siasa za nchi hii. Wakati huo, alikuwa staa wa muziki na jina maarufu alilofahamika nalo ni ‘Mwana FA’.
Tunazungumzia kipindi ambacho alikuwa mmoja ya memba wa Kundi la East Coast ‘Watoto wa Upanga’ akiwa na washikaji zake; King Crazy ‘GK’, AY, Snare, na O-Ten.
Hata wangesimama wote watano, ungeweza kumtambua Mwana FA kwa mwonekano wake wa kibishoo, labda kuliko wengine wote.
Staili yake ya kusuka nywele, uwezo wa kunyuka pamba, achilia mbali rangi ya shombeshombe, vilimfanya awe tofauti kidogo na wenzake hao.
Tofauti na wasanii wengi walioshindwa kusimama kwenye gemu wakiwa bila kundi, Mwana FA aliweza kuwika hata pale alipoachia ngoma zake nje ya East Coast.
‘Mwanafalsafa’, ‘Alikufa kwa Ngoma’, ‘Unanisikiza Mchumba’ na ‘Mabinti’, ambazo kila moja kwa wakati wake iliweza kuwa ‘wimbo wa Taifa’ kwa namna ulivyosikika kila kona ya mtaa.
Kuanzia hapo, Mwana FA alidhihirisha kuwa ubora na uwezo wake hakutugemea nguvu ya kundi. Kwamba angeweza kusimama peke yake na bado ‘akasepa na kijiji’.
Baada ya miaka mingi ya kuuishi ubishioo wa East Coast, historia ilianza kubadilika Oktoba, 2020. Alipojiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kugombea kiti cha katika Jimbo la Muheza mkoani Tanga.
Licha ya uchanga wake kwenye siasa, mizizi ya nguvu ya ushawishi aliyokwishaijenga kupitia sanaa ya muziki iliwasukuma wananchi wa Muheza wamuamini na kumpa ubunge. Akaingia mjengoni Novemba, 2020.
Miaka mitatu tu baadaye, kama ambavyo wachambuzi wanavyoweza kusema bado hakuwa na uzoefu mkubwa, Mwana FA aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akiwa amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitatu tena, leo Novemba 26, 2026, amepiga hatua nyingine kubwa kwenye safari yake kwenye ulingo wa siasa. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua kuwa Waziri wa Uvuvi.
Ukifuatilia, utabaini kuwa Mwana FA amekuwa akipiga hatua kubwa kila baada ya miaka mitatu tangu aanze kujihusisha na siasa za nchi hii. Ubunge [Oktoba 2020], Naibu Waziri Februari, 2023] na sasa Waziri [Novemba 2026].


