NEW YORK, Marekani
MAAMBUKIZI mapya ya ugonjwa wa Ukimwi mwaka 2027 yanatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa [UN].
UN imeeleza kuwa tishio la ongezeko linatokana na mataifa makubwa, ikiwamo Marekani, kusitisha ufadhili kwenye miradi ya kudhibiti ugonjwa huo.
Utafiti huo unakuja wakati UN pia ikieleza kuwa vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kwa kiwango cha kuridhisha kwa miaka 20 ya hivi karibuni.
Aidha, UN inaeleza kwamba Ukimwi ulisababisha vifo takribani 570,000 duniani kote mwaka 2025, sawa na vifo 1,600 kila siku.
Hata hivyo, kwa mujibu wa UN, idadi ni ndogo, ikilinganishwa na vifo 600,000 mwaka 2024 na milioni 1.3 mwaka 2010.
Katika hatua nyingine, UN imeeleza kuwa watu milioni 1.2 walipata maambukizi ya Ukimwi mwaka 2025, hivyo kufanya idadi ya wanaoishi na ugonjwa huo kufikia milioni 41.
Lakini, utafiti huo uliohusisha mataifa 172 ulibaini kuwa watu milioni 32.1 kati ya hao milioni 41 walishaanza kutumia njia za kukinga wengine.


