Na Winfrida Mtoi, Gazetini
TANZANIA inatarajia kupokea shehena ya kwanza ya mafuta ghafi kutoka Uganda kupitia Bandari ya Tanga mwaka 2027, baada ya kukamilika kwa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotekelezwa kwa asilimia 93.9.
Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya nishati Afrika Mashariki, huku Serikali ikilenga kuifanya Tanga kuwa kitovu cha kikanda cha shughuli za kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza mafuta pamoja na bidhaa zinazotokana na mafuta.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema hayo leo, Novemba 24, 2026,Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia matokeo ya ziara ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uganda, iliyofanyika Novemba 18 na 19, mwaka huu.
Amesema mradi wa EACOP unaendelea vizuri, huku kazi kubwa ikiwa imekamilika na maeneo yaliyosalia yakiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, asilimia 6.1 iliyobaki inatarajiwa kukamilika katikati ya mwaka 2027, hatua itakayowezesha kuanza kwa usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Uganda kupitia bomba hilo hadi Bandari ya Tanga.
“Naomba tu niwatoe wasiwasi Watanzania, mradi uko vizuri na unaenda vizuri. Kwa ufupi, mradi unapofikia asilimia 93, sisi tunaosimamia miradi hautupi presha tena,” amesema.
Akizungumzia manufaa mapana ya mradi huo, Prof. Mbarawa amesema moja ya makubaliano yaliyofikiwa katika ziara ya Uganda ni kuharakisha mpango wa kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati Afrika Mashariki.
Amesema mpango huo unahusisha kuendeleza miundombinu ya kuhifadhi mafuta, kuyasafirisha na kusambaza bidhaa za mafuta, pamoja na kuimarisha huduma za usafirishaji na ugavi.
Aidha, amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea, plastiki, kemikali za viwandani na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta, hatua inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali hizo na kukuza shughuli za viwanda nchini.
“Tunataka Tanzania isiwe nchi ya kupitisha mafuta pekee, bali iwe pia kitovu cha shughuli za uchumi zinazohusiana na nishati, viwanda na biashara. Kwa vijana wa Tanzania huu ni mwanzo wa fursa muhimu,” amesema Prof. Mbarawa.


